Habari Mseto

Mkenya anayeishi Dubai asema bila kuvalia barakoa na glavu hakuna kuuziwa chochote

April 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

Wakenya wanapenda kuzuru na kufanya biashara mjini Dubai katika Milki za Kiarabu. Zaidi ya Wakenya 50, 000 wanaishi nchini humo, hasa Dubai.

Wakati huu, mambo ni magumu katika nchi hiyo anavyosimulia Mkenya Lilian Adongo kuwa watu wanafutwa kazi kutokana na janga la virusi vya corona.

“Kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona, mambo hapa Dubai yalikuwa sawa. Watu walitembea bila hofu, na hata kujaa kwenye ufukwe.

Hata hivyo, sasa hivi mambo yamebadilika. Kufikia saa mbili usiku, hakuna mtu anafaa kuwa nje ya nyumba. Ninavyozungumza nawe sasa hivi ni saa tatu usiku; Dubai ni kimya kama maji mtungini.

Hakuna mtu anakubaliwa kununua bidhaa ‘supermarket’ bila kuvalia barakoa na glavu. Bila vitu hivi vyakuzuia maambukizi ya virusi vya corona, huwezi kuuziwa chochote.

Makanisa yote, misikiti, taasisi za elimu na maeneo ya burudani kama vile ya kuona sinema, yalifungwa.

Nimekuwa Dubai kwa miaka mitano sasa. Nilipowasili hapa, nilifanyia kampuni moja kazi, lakini nikajiuzulu kwa sababu mshahara ulikuwa mdogo. Sasa najishughulisha na biashara ambayo nilianzisha baada ya kujiuzulu. Biashara yenyewe ni ya kuuza bidhaa mtandaoni.

Changamoto mpya imejitokeza katika biashara yangu wakati huu wa janga la virus ivy corona. Wateja wameongezeka, lakini hakuna njia ya kuwafikishia bidhaa ni balaa. Nalazimika kutumia mabasi ya bure kusafirisha bidhaa zilizonunuliwa ama niitishe teksi kwa niaba yao halafu wanalipa ada ya teksi wakipokea bidhaa zao.

Jamaa zangu wako Kenya, lakini naishi pekee yangu hapa Dubai. Ningependa kusihi Wakenya wajiweke salama wasije wakaambukizwa virusi hatari vya corona. Pia, nawashauri wasijaribu kuomba kazi wakati huu. Wasijaribu kutafuta kazi yoyote kupitia kwa maajenti kwa sababu wataliwa pesa bure. Vilevile, wasijaribu kuja na visa ya kutalii kwa sababu hakuna kazi. Watu wengi wamepoteza kazi kwa njia ya kufutwa bila ya kulipwa mishahara yao. Sasa hivi ni kubaya kabisa.”

Milki za Kiarabu imethibitisha watu 2, 659 katika nchi hiyo wameambukizwa virusi vya corona, ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Covid-19. Watu 12 wamefariki nchini Milki za Kiarabu kutokana na ugonjwa huo. Virusi hivyo, ambavyo vilianzia mjini Wuhan nchini Uchina, vimeenea katika mataifa 209.