Habari Mseto

Mkenya anayeishi London asema kila mtu anafanyia kazi nyumbani

April 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

Njuguna ni mkazi wa East London nchini Uingereza. Ameishi katika nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 20. Yeye ni mmoja wa waathiriwa wa maambukizi ya virusi vya corona.

Kufikia wakati wa kuandika makala haya, Uingereza ilikuwa imethibitisha visa 65, 077 vya maambukizi, huku watu 7, 978 wakifariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.

Njuguna alisimulia Taifa Leo Dijitali jinsi wakazi wa Uingereza wameathirika na janga la corona na pia anachodhani kitafanyika baada ya janga hili kumalizika na mengine mengi. Mzawa huyu wa Kenya alilazimika kujitenga mwezi Machi katikati baada ya kuambukizwa, lakini sasa yuko sawa.

“Hapa Uingereza, kila mtu anapewa nafasi sawa bila ya kujali anakotoka, hata kama ni Mkenya. Kama wewe hauko katika mstari wa mbele katika vita vya kupigana na virusi hivi na pia huduma zako hazihitajiki na jamii, unafaa kufanyia kazi nyumbani. Tunatoka kwa nyumba wakati pekee tunataka kununua chakula, dawa/kupata matibabu, ama kufanya mazoezi mara moja kwa siku.

Maafisa wa polisi wamepewa mamlaka ya kuzuia watu kusafiri, na treni zinatumiwa tu na wale wanaoenda kazini. Bila ya kuficha chochote, maisha ni magumu, hasa kwa wale wanaolipwa kulingana na saa walizofanya kazi na pia wale ambao huduma zao hazihitajiki. Inamaanisha kuwa lazima waombe kusaidiwa na serikali. Hata hivyo, Wakenya wengi hapa wanatoa huduma muhimu za utunzaji kumaanisha wako kazini.

Kwa mujibu wa ripoti, watu wanaofanya kazi katika hospitali na nyumba za kutunza watu wasiojiweza wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa kwa sababu kuna uhaba wa mavazi maalum ya kujikinga. Kuna Wakenya kadhaa hapa walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Wakenya pia wanafanya kazi kwa saa nyingi.

Zaidi ya watu 7,000 walikuwa wamepoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini humu hapo Aprili 9. Idadi hii ni ya wale waliofariki wakiwa hospitalini na wala si nyumbani ama katika makao maalum ya kutunza watu. Waziri wetu mkuu ametoka katika chumba cha watu mahututi leo jioni.

Ningependa kutoa ushauri kwa Wakenya kuwa wasalie nyumbani. Wasisafiri ovyoovyo. Tafadhali msitembelee jamaa zenu ambao ni wakongwe wakati huu kwa sababu wao ndio wako katika hatari zaidi ya kupata virusi hivi. Usicheze na ugonjwa huu; utakupeleka jongomeo kwa siku chache. Kama wewe ni mdhoofu, huwezi kupelekwa hospitali. Kama wewe ni mzee sana, jukumu la kuamua unaishi ama la liko mikononi mwa madaktari kwa sababu hakuna mashine za oksijeni za kutosha katika hospitali. Hospitali pia zina kiasi kidogo cha oksijeni.

Mimi ni meneja katika shirika la huduma za kijamii. Nafanyia kazi nyumbani na kusimamia huduma hizo kutoka nyumbani. Ni kazi ngumu kubadilisha jinsi umezoea kufanyia kazi ofisini na kuifanyia nyumbani kila siku. Inachosha sana.

Tamaduni ya Uingereza inatuhitaji kuwa na mtazamo mzuri na kama jamii, tunaungana kusaidia serikali. Tumekuwa tukiwapatia moyo wafanyakazi wetu kutoka Shirika la Afya la Kitaifa (NHS) kwa sababu wanafanya kazi kubwa kuokoa maisha.

Wacha nikushangaze kuwa mara tu watu waliambiwa wafanyie kazi nyumbani, karibu kila mtu alikubali. Mashirika mbalimbali yalianza kupanga jinsi watu wanaweza kuchangia kwa kufanyia kazi nyumbani.

Na ninakuhakikishia kuwa tunafanya kazi kubwa sana nyumbani kuliko tunapokuwa ofisini. Naamini mashirika mengi yataiga mpango huu baada ya janga la virusi vya corona kuisha ili kupunguza gharama zao.

Mtoza ushuru amekubali kulipa kila mtu Sh793 (pauni 6) kwa kufanyia kazi nyumbani hapa Uingereza. Mashirika yanayohudumia watu kutoka saa nne asubuhi na kufunga saa mbili usiku yanakubaliwa kutumia teksi hadi nyumbani kama hawatumii magari yao kwa sababu idadi ya treni na mabasi imepunguzwa sana ili kuepuka mikusanyiko ya watu wengi.

Nikimalizia ni kuwa, kuna ripoti kuwa watu wengi pia wamepoteza kazi zao nchini humu kwa sababu ya janga hili.”