Mkutano wa kusuluhisha utata eneo la Kapedo watibuka
WYCLIFF KIPSANG na FLORAH KOECH
MKUTANO wa amani ambao ulipangwa kufanyika kati ya viongozi wa Turkana na Pokot mnamo Jumatatu ili kutatua mzozo kuhusu Kapedo, ulifutiliwa mbali dakika za mwisho huku taharuki ikitanda katika eneo hilo.
Mkutano huo uliotarajiwa kufanywa Kapedo katika mpaka wa Kaunti za Baringo na Turkana ulifutiliwa mbali kwa kuwa viongozi wa jamii hizo mbili walikuwa wanabishana.
Duru jana zilisema taharuki zilizozidi kuhusu eneo hilo lenye mali nyingi ya asili ndizo zilifanya mkutano kutibuka.
Ilisemekana taharuki ilisababishwa na matamshi yaliyotolewa na Mbunge wa Tiaty William Kamket wiki iliyopita, ambapo alidai eneo linalozozaniwa lipo katika eneobunge lake.Dai hilo halikupokewa vyema na wenzake wa Turkana.
Gavana wa Baringo, Bw Stanley Kiptis ambaye alikuwa amepangiwa kusimamia mkutano huo na mwenzake wa Turkana, Bw Josphat Nanok, jana alithibitisha mkutano ulifutiliwa mbali ili kutoa wakati wa kutuliza taharuki katika eneo hilo.
“Tumeamua kuahirisha mkutano huo ili kuwezesha viongozi wa maeneo hayo mawili kupata mwafaka. Baadhi ya viongozi hivi majuzi walitoa matamshi ambayo yalisababisha taharuki katika eneo hilo,” akasema.