Habari Mseto

Mlima Kenya waraiwa kuikaribisha Akamba katika Gema

April 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

JAMII za Mlima Kenya zimeraiwa kuiunga mkono kisiasa jamii ya Akamba kwa kuikaribisha tena kwenye ubinamu wa jamii za GEMA (Gikuyu, Aembu na Ameru).

Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana, alisema kuwa imefikia wakati jamkii hizo ziikaribishe upya jamii ya Akamba, ili kurejesha umoja ambao ulikuwepo awali.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatano, Prof Kibwana alisema kuwa jamii hiyo (Akamba) itawatuma wazee kwa jamii hizo tatu kuwasilisha rasmi ujumbe wa kuomba ukaribisho mpya wa kisiasa.

“Lazima turudishe ushirikiano uliokuwepo awali. Vilevile, ni wakati wenzetu kutoka Mlima Kenya kutuunga mkono pia kisiasa kama vile ambavyo tumekuwa tukiwaunga viongozi wao,” akasema Prof Kibwana.

Jamii ya Akamba ilijitoa kwenye ubinamu huo, ikilalamikia “ubinafsi na usaliti wa kisiasa.

Wakati huo huo, magavana wa eneo la Ukambani wameanza kushauriana kuhusu njia za kubuni mkakati wa pamoja kwenye vita dhidi ya virusi vya corona.

Prof Kibwana alisema kuwa wanapanga kufanya mkutano na magavana Alfred Mutua (Machakos) na Charity Ngilu (Kitui) ili kuona vile wataunganisha juhudi zao kwenye harakati hizo.

Baadhi ya juhudi hizo ni kubuni ushirikiano kwenye ukaguzi wa watu ikiwa wameambukizwa virusi, utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kuwalinda wananchi dhidi ya kuambukizwa na uhamasishaji wa umma kuhusu njia za kujilinda.

Nguzo kuu

Prof Kibwana alisema kuwa ushirikiano wa kaunti ndio utakuwa nguzo kuu katika kupiga jeki harakati zinazoendeshwa na Serikali ya Kitaifa kwenye vita dhidi ya virusi.

“Lazima kaunti zote ziungane kupitia miungano ya kiuchumi ili kuisaidia Serikali ya Kitaifa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo. Hivyo ndivyo tutafaulu kulikabili janga hili,” akasema.

Kaunti hiyo haijarekodi kisa chochote cha maambukizi ya corona.

Wakati huo huo, gavana anazitaka kaunti kukuza utalii asilia, ili kuimarisha mapato yake.

Alisema kuwa lazima ziwahamasishe Wakenya kuzuru maeneo mbalimbali ya utalii ncnini, badala ya kuwategea raia wa kigeni.

Alieleza kuwa hilo ndilo litaziwezesha kujisimamia kifedha, ikiwa janga lingine kama corona litatokea tena katika ziku za usoni.

“Kwa kupigia debe na kukuza utalii asilia, hilo litahakikisha kuwa tunapata mapato yetu kwa urahisi, badala ya kutegemea raia wa kigeni, ambao hawako kwa sasa,” akasema.

Katika juhudi za kukabili corona, kaunti imeanza mpango kuwafunza zaidi ya watu 40,000 ili kuwaelimisha wananchi kuhusu njia za kujilinda dhidi ya virusi.