Habari Mseto

Mlinzi wa gavana auawa na bodaboda sababu ya deni la Sh100

December 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WANYORO

AFISA wa ulinzi wa Gavana wa Embu Martin Wambora aliyeuawa Jumanne baada ya mzozo kuibuka na wahudumu wa bodaboda kuhusu nauli ya Sh100.

Bw Christopher Njue, 44, ambaye ni mlinzi wa Gavana Wambora alichapwa na wahudumu hao wa Bodaboda katika eneo la Kithimu, baada ya afisa huyo kusisitiza kuwa alitaka kulipia huduma kwa njia ya Mpesa.

Kaimu chifu wa kata ya Kithimu Albert Njiru alisema kisa hicho kilitokea saa nane usiku na kuwa ni polisi waliokuwa wakipiga doria ambao walimpata afisa huyo akiwa katika hali mbaya na kumpeleka katika hospitali ya Embu Level Five ambapo majeraha yalimzidia na akafa.

“Walitofautiana kuhusu mbinu ya malipo na wahudumu hao wa bodaboda ambao waliungana na kuanza kumpiga na vifaa butu. Polisi walimpata akiwa hali mahututi,” Bw Njiru akasema.

Polisi baadaye walimkamata mshukiwa mmoja na kumzuilia katika kituo cha polisi cha Itabua.

Tangu kisa hicho kutendeka, wahudumu wengi wa Boda boda wametoroka maeneo ambapo huwa wanafanyia kazi ili kuepuka kukamatwa.

Wafanyakazi wenza wa Bw Njue walimtaja kuwa mtu mtulivu na afisa aliyejitolea kazini.

“Alikuwa mwanaume mcheshi. Alikuwepo wakati gavana alikuwa na hafla katika ofisi yake Jumatatu,” akasema mfanyakazi mwenzake.

Katika siku za hivi majuzi, wahudumu wa bodaboda wamekuwa wakiangaziwa kuhusiana na utovu wa nidhamu katika shughuli zao, kukiuka sheria kwa kuchukua sheria mikononi mwao wanapokosewa na raia.

Serikali inapanga kuanza kutekeleza mwongozo uliotolewa na jopo maalumu lililoundwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, mwaka ujao ili kutambua wahudumu wote wa bodaboda kama njia ya kudhibiti sekta hiyo iliyokua kwa kasi.