• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Mmiliki wa bwawa la Solai azuiliwa kusafiri ng’ambo

Mmiliki wa bwawa la Solai azuiliwa kusafiri ng’ambo

Na RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kampuni za Solai zilizojenga bwawa la Solai ambalo lilipasuka na kusababisha vifo vya watu 47 amezuiliwa na mahakama kusafiri hadi kesi ya fidia aliyoshtakiwa isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Antony Ombwayo alimwamuru Bw Patel Mansukhlal Kansagra asisafiri ng’ambo hadi kesi dhidi yake na washtakiwa wengine isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Ombwayo alifahamishwa kuwa endapo Bw Kasangra atasafiri na kukataa kurudi nchini basi kesi iliyowasilishwa na wahasiriwa wa mkasa huo wa bwawa la Solai itasambaratika.

Walalamishi hao wanaomhakama mahakama iamuru Bw Kasangra na washtakiwa wengine washurutishwe kuwalipa fidia.

Wakili Ronald Onyango ameomba mahakama iamuru  Bw Kasangra awasilishe mahakamani Sh5bilioni za kugharamia fidia ya wahasiriwa endapo mshtakiwa atakubaliwa kusafiri ng’ambo.

Katika kesi hiyo Bw Kasangra ameshtakiwa pamoja na Solai Group of Companies, Kensalt Limited, Patel; Coffee Estate Limited, Vinoj Coffee Estate, Vinoj Jaya Kumar Mamlaka ya  Maji Nchini (WRA), Mamlaka ya kitaifa kuhusu mazingira (NEMA), Mamlaka ya Ujenzi Nchini ( NCA) na Mwanasheria mkuu.

Bw Onyango amesema katika kesi aliyowasilisha kuwa washtakiwa wenzake Bw Kasangra wanategemea yeye na kutoroka kwake nchini kutayumbisha kabisa kesi hiyo.

Wakili huyo anasema kuwa mkasa huo wa Mei 9, 2018 ulisababisha jamii nyingi kutoweka.

“Ikiwa mshtakiwa huyu atakuwa anakubaliwa kusafiri ng’ambo anapasa kushurutishwa kuwasilishwa kortini Sh5 bilioni za kugharamia malipo ya fidia ya wahanga wa mkasa huo,” korti iliombwa.

Mshtakiwa huyu pamoja na washukiwa wengine wanakabiliwa na mashtaka ya kusababisha vifo vya watu 47 katika mkasa huo wa bwawa.

Bwawa hilo lilipasuka na kusomba mali na kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Solai kaunti ya Nakuru.

Bw Onyango alieleza mahakama kuwa kuna kesi mbili dhidi  ya mshtakiwa. Moja ya kushurutishwa alipe fidia na nyingine ya kusababisha vifo vya watu.

Mahakama ilijulisha kesi dhidi ya Kasangra iko na umuhimu mkubwa kwa umma.

You can share this post!

#FreeBobiWine: Maandamano jijini Kampala yachacha

BI TAIFA JUNI 19, 2018

adminleo