Habari MsetoSiasa

Moses Kuria sasa aomba radhi baada ya kumlaumu Uhuru

January 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

MARY WAMBUI Na BENSON MATHEKA

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, Ijumaa alilazimika kumuomba msamaha Rais Uhuru Kenyatta kwa matamshi aliyotoa mkesha wa mwaka mpya akimlaumu kwa kupuuza eneo la Kati licha ya wakazi kumpigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Akihutubu katika uwanja wa michezo wa Thika katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya, Bw Kuria aliwataka wakazi kutafakari kabla ya kupiga kura ili wasiwe wakikosa miradi ya maendeleo licha ya kupiga kura kwa wingi.

“Mimi nataka kusema hivi, tukivuka mwaka wa 2019 nyinyi mfikirie sana. Sisi mambo yetu ni kupiga kura; baada ya kupiga kura maendeleo tunapatiana kwingine. Hiyo ujinga tuwache,” alisema Bw Kuria.

Matamshi hayo yalimfanya ashutumiwe vikali na viongozi wa eneo hilo, akiwemo mwakilishi wa wanawake Gathoni Wamuchomba, aliyekuwa gavana William Kabogo na baraza la wazee wa Agikuyu.

Viongozi hao walisema Rais ameanzisha miradi mingi na kwamba Kuria alikuwa akiwapotosha watu na kumkosea heshima Rais Kenyatta.

Lakini jana, mbunge huyo alisema alielekeza ujumbe wake wa mwaka mpya kwa viongozi wa Kaunti ya Kiambu ambao wanaangazia miradi ya kumaliza ulevi, kama ya pekee ambayo Rais anafaa kuzindua akitembelea eneo hilo.

Akihutubia wanahabari eneo la Kimunyu, Gatundu Kusini, Bw Kuria alisema ameomba msamaha kila mtu aliyeelewa visivyo matamshi yake, akiwemo Rais Kenyatta na akawataka viongozi kuacha kuzua uhasama kati yake na Rais.

“Sijawahi kumdharau Rais. Hata hivyo, tamko lolote nililotoa likaeleweka vibaya ninaomba msamaha kwa Rais na mtu mwingine yeyote yule,” alisema Kuria.

Bw Kuria alikiri kwamba kwa kweli kuna miradi mingi ya maendeleo iliyoanzishwa na serikali lakini akasema viongozi, hasa wa Kaunti ya Kiambu walikuwa wakitoa taswira mbaya kwa kumwalika Rais katika shughuli za kurekebisha walevi pekee.

Matamshi yake ya jana, yalijiri saa chache baada ya baraza la wazee wa jamii ya Agikuyu kutoka Gatundu Kusini kujitenga na ujumbe wake wa mwaka mpya na kumtaka kumuomba Rais msamaha.

Wazee hao alisema wanatambua ajenda ya maendeleo ya Rais na kwamba ameanzisha miradi mingi ya maendeleo kote nchini ikiwa ni pamoja na eneo lao la Gatundu Kusini.