Mpango wa mbolea ya bei nafuu umetekwa na wakora, EACC sasa yafichua
MPANGO wa serikali wa kutoa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima, mojawapo ya nguzo kuu za Ajenda ya Rais William Ruto ya kuwainua wananchi wa pato la chini umevurugwa na magenge ya walaghai na wafanyabiashara matapeli, ripoti mpya ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) imefichua.
Kulingana na ripoti EACC, mianya katika usimamizi wa mpango huo ilifungua njia ya wizi, ulaghai na usambazaji wa mbolea duni, hali iliyowaacha maelfu ya wakulima katika dhiki.
Mpango huo uliozinduliwa mwaka 2023 ulilenga kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza utoshelevu wa chakula nchini.
Hata hivyo, ripoti hiyo ya Septemba iliyoonwa na gazeti la Taifa Leo inaonyesha jinsi maafisa wa serikali walivyoshindwa kusimamia utekelezaji, na hivyo kuruhusu walanguzi kupenya katika kila hatua kuanzia usajili wa wakulima, ununuzi, maghala hadi usambazaji.
Mfumo wa kidijitali wa usajili wa wakulima (KIAMIS), uliruhusu usajili wa mara nyingi kwa mkulima mmoja.
Jambo hilo lililotumiwa vibaya na matapeli kujipatia vocha nyingi huku wakulima wadogo wakiachwa nje.
EACC inasema baadhi ya maafisa wa kilimo wa wadi hawakuwa na vifaa wala usafiri wa kutembelea mashamba, hali iliyowafanya kutegemea fedha kutoka kwa wakulima.
Hilo liliwawezesha walaghai kuficha vocha na kuuza mbolea hiyo kwa bei ya juu.
Katika msimu wa mvua ndefu wa Machi–Mei 2024, kampuni moja iliyopewa jina la siri “XXX Chemicals Ltd” ilisambaza magunia 69,070 ya mbolea aina ya NPK 10:26:10 ambayo Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS) baadaye lilibaini kuwa haikufikia viwango vinavyohitajika.
Wakati huo tayari magunia 67,761 yalikuwa yameuzwa kwa wakulima 13,633.
Ripoti hiyo pia inasema magunia 27,518 ya mbolea kutoka kampuni nyingine yalizuiliwa baada ya kugunduliwa kuwa na muda mfupi wa matumizi, lakini Bodi ya Kitaifa Nafaka na Mazao (NCPB) bado iliagiza mzigo mwingine kutoka kwa kampuni hiyo.
EACC inasema udhaifu wa usimamizi wa hesabu, ukosefu wa mifumo ya kielektroniki na ufuatiliaji hafifu uliwapa nafasi wezi na walaghai kuiba fedha za umma.
Wakulima wengi walijikuta wakikosa mbolea licha ya kujisajili, huku baadhi yao wakilazimika kununua kutoka kwa madalali kwa bei ya juu.
Ripoti hiyo inapendekeza serikali kuanzisha mifumo ya kielektroniki kikamilifu, kufadhili ipasavyo maafisa wa kilimo wa wadi, na kuhakikisha mashirika kama KEBS, KEPHIS na KALRO yanahusishwa katika kila hatua ya ukaguzi wa ubora wa mbolea.
EACC inatahadharisha kuwa bila mageuzi hayo, mpango wa ruzuku ya mbolea utazidi kuwa shamba la ufisadi, na mzigo wake kuendelea kuwabebesha wakulima wadogo wa Kenya.