Msaada wa corona haukuibwa, Kagwe sasa asema
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe sasa amebadilisha msimamo na kukana madai kwamba sehemu ya shehena ya msaada wa vifaa vya kupambana na Covid-19 vilivyopewa Kenya na Wakfu wa Jack Maa viliibwa.
Hata hivyo Bw Kagwe aliwaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya kwamba wizara yake ilialika Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ,kuanzisha uchunguzi “baada ya uvumi kuenea kwamba baadhi ya vifaa hivyo viliibwa.”
Mnamo Juni mwaka huu, Bw Kagwe alikiri hadharani akiwa Nyeri kwamba watu aliowataja kama wezi walishirikiana na maafisa wa wizara yake kuiba sehemu kubwa ya vifaa hivyo.
“Inasikitisha kuwa maafisa fulani katika Wizara yangu wameshirikiana na kuiba sehemu ya vifaa kutoka kwa wakfu wa Jack Ma. Walifanya wizi huo katika uwanja wa JKIA hata kabla ya kuwasilishwa kwa hospitali husika. Uchunguzi umeanzishwa na naamini kwamba watapatika na kuadhibiwa,” akasema Bw Kagwe wakati huo.
Shehena ya kwanza ya vifaa hivyo iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), mnamo Machi 24, 2020 na vilijumuisha barakoa 100,000 na seti 20,000 za vifaa vya kupima virusi vya corona.
Lakini licha ya Waziri Kagwe jana kukana madai kuhusu wizi wa baadhi ya vifaa hivyo, Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Dkt Chris Obure alifurushwa kutoka kwa kikao cha kamati hiyo kwa kutoa maelezo kuhusu suala hilo ambayo hayakuwaridhisha wabunge.
Dkt Obure ambaye alikuwa amemwakilisha Waziri wa Uchukuzi James Macharia, alifeli kutoa maelezo kuhusu idadi ya kamili ya vifaa vilivyopokewa katika uwanja wa JKIA, na ile iliyowasilishwa kwa Wizara ya Afya na asasi husika.
Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Kupitisha Bidhaa zinazoingizwa nchini, Bw Felix Ateng kutoa maelezo ambayo yalikinzana na yale ya Dkt Obure.
“Naamuru muondoke mkaoanishe maelezo yote tunayohitaji kisha mrejee hapa kesho (leo) saa tatu asubuhi. Inaonekana wazi kwamba hamkuwa mumejiandaa kutoa maelezo yote ambayo tulitaka,” akasema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi Sabina Chege.