Mshangao wanaharakati wakidai shule inapanga kuiba KCSE
WAANAHARAKATI wawili kutoka Kaunti ya Homa Bay wameliandikia Baraza la Kitaifa la Mtihani Nchini (KNEC) ili lichunguze shule moja ya upili eneo la Suba Kusini kutokana na madai kuwa inapanga kushiriki udanganyifu kwenye Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE).
Wanaharakati hao wamemtaka Afisa Mkuu wa KNEC na afisa wa nyanjani wafuatilie shughuli za shule hiyo baada ya wazazi kutakiwa kulipa ada isiyoeleweka mtihani wa KCSE ukianza Jumatatu.
Evans Oloo na Eugene Obisa ambao ni wanaharakati wanasema kukusanywa kwa pesa hizo kunashangaza na huenda zikatumiwa kusaidia katika wizi wa mtihani.
“Kuna mpango wa kuvuruga uwazi katika mtihani huo kwa sababu pesa ambazo zinakusanywa, matumizi yake hayafahamiki,” akasema Bw Oloo kwenye barua hiyo.
Hapo nyuma, Wizara ya Elimu iliorodhesha baadhi ya kaunti ambazo ilidai kuna mipango inayosukwa ya wanafunzi na walimu kushiriki udanganyifu kwenye mtihani wa KCSE. Homa Bay ni kati ya kaunti ambazo ziliorodheshwa.
Kwa mujibu wa Bw Oloo, baadhi ya walimu katika shule hizo waliibua suala hilo wakisema usimamizi una mpango wa kuwasaidia wanafunzi kupita mtihani wao.
Bw Oloo aliongeza kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo anashiriki mpango huo vilivyo ambapo wazazi wametakiwa kulipa Sh3,000.
“Wanasema pesa hizo ni za kusaidia kuhakikisha wanafunzi wapo kwenye mazingira mazuri wanapofanya mtihani wao. Hili ni suala ambalo linaibua madai mengi kwa sababu ni mazingira gani sasa wanafunzi wanahitaji kuliko yale ambayo wamekuwa wakiyasomea?” akasema Bw Oloo kwenye barua yake.
Wanaharakati hao walisema walimu ambao walipinga ada hiyo walipuuzwa na wakata KNEC iangazie suala hilo na pia kufuatilia shule za kaunti za Homa Bay.
“Tunaomba uchunguzi kuhusu suala hili kwa sababu hatutaki matokeo ya watahiniwa yafutiliwe mbali. Mwalimu Mkuu wa shule hiyo achunguzwe na achukuliwe hatua iwapo itabainika ana njama ya kuwasaidia wanafunzi kushiriki wizi wa mtihani,” akasema.