Mshukiwa wa nne wa wizi wa mabavu afikishwa kizimbani
Na RICHARD MUNGUTI
SIKU arobaini zilitimia pale mshukiwa wa nne aliposhtakiwa Jumanne kwa kumshambulia na kumnyang’anya kimabavu mfanyabiashara Sh100,000 katika hoteli moja jijini Nairobi Aprili 30, 2018.
Bw Brian Shem Owino alifikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi. Alikanusha alimnyang’anya kimabavu Timothy Muriuki Sh100,000 katika hoteli ya Boulevard.
Shtaka lilisema wakati wa wizi huo mlalamishi alijeruhiwa.
Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kuwa kesi dhidi ya Bw Owino iunganishwa na nyingine dhidi ya Mbunge anayewakilisha Kenya katika bunge Afrika Mashariki (EALA) Simon Mbugua aliye na Mabw Antony Otieno Ombok almaarufu Jamal na Benjamim Odhiambo Onyango almaarufu Odhis walifikishwa kortini baada ya patashika kadhaa kati ya polisi na washikadau wa haki waliotaka haki ifanywe na waliomshambulia Bw Timothy Muriuki wachukuliwe hatua kali.
Polisi waliwatia nguvuni watatu hao Mei 8 na kuwafungulia mashtaka.
Kisa hiki cha kushambuliwa kwa Bw Muriuki kilipeperushwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Washtakiwa waliomba waachiliwe kwa dhamana kupitia kwa mawakili Cliff Ombeta, Harun Ndubi, Nelson Havi na Michael Osundwa.
Ijapokuwa ombi hilo lao halikupingwa na kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha , hakimu mwandamizi Martha Mutuku aliombwa awaachulie kwa masharti makali ikitiliwa maanani Bw Mbugua yuko na ushawishi mkubwa na atavuruga mashahidi.
Lakini Bi Mutuku aliwaachilia kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu akisema “hakuna ushahidi uliowasilishwa kuonyesha kwamba washtakiwa wako na uhusiano na mashahidi.”
Korti ilisema mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji anatakiwa kuwasilisha ushahidi kuhusu madai yanayotolewa kortini badala ya kuacha korti “ itegemee uvumi.”
Korti iliorodhesha kesi hiyo kusikizwa Julai 17.
Hakimu aliamuru kila mmoja wa washukiwa hao apewe nakala za mashahidi aandae utetezi wake.