Habari MsetoSiasa

Msiingize siasa katika BBI, viongozi wa kidini waonya

January 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BARNABAS BII

VIONGOZI wa dini kutoka eneo la Bonde la Ufa wanataka mjadala kuhusu ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) utenganishwe na siasa za 2022.

Viongozi hao wanasema kuwa kuchanganywa kwa siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 na ripoti ya BBI kumezua joto la kisiasa nchini.

Wakiongozwa na Askofu Dominic Kimengich wa Parokia ya Kanisa Katoliki la Eldoret, viongozi hao walisema kuwa baadhi ya wanasiasa wanalenga kutumia ripoti ya BBI kujipatia umaarufu wa kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mjadala kuhusu BBI tayari umeanza kutenganisha nchi. Ripoti ya BBI isichanganywe na siasa za 2022 kwani kufanya hivyo nchi itagawanyika zaidi kwa misingi ya kikabila,” akasema Kimengich.

Alisema nchi inakabiliwa na changamoto tele zinazohitaji kupewa kipaumbele kama vile ufisadi, dhuluma za kihistoria na kuzorota kwa uchumi.

“Ripoti ya BBI inalenga kunufaisha Wakenya wote na wala si chombo cha wachache kuingia mamlakani. Nchi haijapona kutokana na machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyosababisha maafa miaka iliyopita. Viongozi wa kisiasa wanafaa kuwa waangalifu wanapojadili ripoti ya BBI,” akasema Askofu Kimengich.

Akaendelea: “Ni makosa kwa baadhi ya wanasiasa kulazimisha Wakenya kuunga mkono ripoti hiyo kwani ni kinyume na misingi ya demokrasia. Kuna masuala nyeti yanayofaa kupewa kipaumbele badala ya kuzungumzia BBI kila uchao.”

Maaskofu wa Kanisa Anglikana (ACK) Dkt Paul Korir wa Parokia ya Kapsabet na Dkt Emmanuel Kimengich wa Parokia ya Kitale waliwataka wanasiasa kuwaacha Wakenya kujifanyia uamuzi kuhusiana na ripoti ya BBI.

“Viongozi walio serikalini na katika upinzani wazike tofauti zao na waache Wakenya wajisomee na wajifanyie maamuzi kuhusu ripoti ya BBI,” akasema Askofu Korir.

Dkt Kimengich alionya wanasiasa dhidi ya kutumia ripoti ya BBI kwa ajili ya masilahi yao ya kibinafsi.

Ripoti ya BBI imezua uhasama mkubwa baina ya wanasiasa wanaoegemea upande wa handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga na wale wanaounga Naibu wa Rais William Ruto.

Mwenyekiti wa ODM tawi la Elgeyo Marakwet Micah Kigen alisema kuwa makongamano ya kujadili ripoti ya BBI ambayo yamekuwa yakiandaliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yanalenga kuhamasisha Wakenya kuisoma na kujifanyia maamuzi bila kushurutishwa.

“Tunataka kutumia mikutano ya BBI kuwezesha Wakenya kusoma ripoti na kisha wafanya uamuzi wao,” akasema.

Alisema kuwa mipango ya kutaka kuandaa mkutano wa kujadili ripoti ya BBI katika ukanda wa Bonde la Ufa inaendelea.

“Wananchi wanahitaji muda wa kutosha wasome na kuelewa ripoti bila kushawishiwa. Tunachofanya ni kuwapa fursa ya kujadili masuala muhimu yaliyomo kwenye ripoti na kisha wajifanyia maamuzi,” akasema Bw Kigen.

Wakati huo huo, chama cha Kanu kimesema kuwa kinataka kuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha Wakenya kusoma ripoti ya BBI.

“Tayari tumeunda sekretariati itakayohakikisha kuwa Wakenya wanasoma ripoti ya BBI na kuielewa vyema,” akasema Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat.