Mswada mpya jikoni kuruhusu NYS kuhudumu KDF
Na VALENTINE OBARA
BARAZA jipya litakalobuniwa kusimamia Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS), litapewa mamlaka ya kuamua kuwatuma vijana wakahudumu katika kikosi cha Jeshi la Taifa (KDF) wakati wa vita ikiwa Mswada wa NYS 2018 utapitishwa bungeni na kuidhinishwa kuwa sheria.
Kwa sasa, Sehemu ya 17 kwenye Sheria ya NYS (2012) imempa rais mamlaka moja kwa moja kuagiza vijana wa NYS wakatumikie KDF endapo nchi itakumbwa na vita, mapinduzi au hali ya tahadhari ya kiusalama.
Lakini mswada uliopendekezwa na Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia na ukakubaliwa katika baraza la mawaziri wiki iliyopita, umemwondolea rais mamlaka hayo.
Mswada huo unasema kutakuwa na baraza ambalo limekabidhiwa majukumu makubwa ikiwemo kuamua kutuma NYS wakatumikie katika vikosi vya jeshi.
Uamuzi wa kuwatuma vijana vitani utatolewa baada ya mashauriano kati ya Baraza la NYS na Baraza la Usalama wa Kitaifa ambalo rais ndiye mwenyekiti wake huku naibu rais akiwa mmoja wa wanachama.
“Endapo sehemu yoyote ya NYS itaagizwa kuhudumu katika KDF au kwa njia nyingine katika ulinzi wa taifa ndani au nje ya Kenya, sehemu hiyo ya NYS itachukuliwa kuwa sehemu ya KDF na itasimamiwa kwa msingi wa sheria zote zinazohusu KDF,” mswada huo unaeleza.
Baraza la NYS litasimamiwa na mwenyekiti atakayeteuliwa na rais.
Wanachama wake watajumuisha Mkuu wa KDF, Mwanasheria Mkuu, katibu wa wizara inayosimamia masuala ya NYS, katibu wa Wizara ya Usalama wa ndani na katibu wa Wizara ya Fedha. Wote watakuwa huru kuteua maafisa kuwawakilisha katika baraza hilo.
Zaidi ya haya, kiapo cha vijana wanaohitimu katika NYS pia kitabadilishwa ili kifanane na cha wanajeshi kwa kuapa kuwa waaminifu na wazalendo kwa rais aliye amiri jeshi mkuu.
Kiapo cha sasa kilicho kwenye Sheria ya NYS kina aya moja pekee ambapo vijana wanaohitimu huapa kuwa waaminifu kwa shirika hilo.
Lakini kiapo kilicho kwenye mswada unaosubiriwa kuwasilishwa bungeni kina aya nne zinazofanana na kiapo cha wanajeshi. Aya mbili za kwanza zinahusu uaminifu kwa rais wa taifa.
, cha tatu kinahusu heshima kwa sheria za NYS na cha nne ni kuhusu utoaji huduma inavyohitajika bila uoga, mapendeleo wala nia mbaya.
Serikali imekuwa ikihamasisha umma kuhusu mswada huo mpya kwa msingi kuwa ukipitishwa utasaidia kuboresha huduma za NYS na usimamizi wake ili kukabiliana na sakata za ufisadi ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika shirika hilo kwa miaka kadhaa sasa.