• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Mswada wa afya ya uzazi waendelea kuibua cheche

Mswada wa afya ya uzazi waendelea kuibua cheche

Na CHARLES WASONGA

MAAKOFU wa Kanisa Katoliki wametofautiana na wanachama wa makundi ya kijamii watetea haki za afya ya uzazi zinazopendekezwa katika Mswada wa Afya ya Uzazi, 2020 ulioko katika Seneti.

Mswada huo ambao unadhaminiwa na Seneta wa Nakuru Susan Kihika umeibua hisia mseto kuhusu kipengele kinachopendekeza uavyaji mimba wakati afya ya mama iko katika hatari pekee. Pendekezo hili linalenga kufanikisha hitaji la kipengee cha 26 (4) cha Katiba kinachokubali kusitisha kwa mimba kutokana na sababu za kiafya.

Katika taarifa iliyosomwa wakati wa ibada ya Jumapili, chini ya Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB) viongozi hao wa kidini wamesema watapinga mswada huo kutokana na kipengee hicho kinachoenda kinyume cha haki ya uhai.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya maaskofu wenzake, Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nakuru Maurice Muhatia amesema watapinga sehemu za mswada huo zinazopendekeza elimu ya ngono kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 18.

“Mswada huo unaenda kinyume na Katiba, haki ya maisha na kulindwa kwa watoto na familia dhidi ya maovu ya kijamii,” Askofu Muhatia amesema.

Akaongeza: “KCCB itaitikia mwaliko kutoka kwa Seneti ili ielezee msimamo wa Kanisa Katoliki na kupendekeza marekebisho ambayo inataka yafanyiwe mswada huo.”

Askofu Muhatia amesema kanisa hilo litajizatiti kutetea haki ya uhai na maadili bora miongoni mwa watoto na watu wa familia.

“Vilevile tutahimiza Wizara ya Elimu na Taasisi ya Kuunda Mitaala (KICD) kuandaa mtaala bora wa mafunzo ya uzazi kwa wanafunzi. Mtaala ambao hauwezi kutumiwa kuvuruga maadili yao,” akaeleza.

Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za kijamii chini ya mwavuli wa “Centre for Reproductive Right” yamewasuta viongozi wa Kanisa Katoliki kwa kupotosha umma kuhusu yaliyomo kwenye mswada huo.

Mkurugenzi wa Shirika hilo anayesimamia Ukanda wa Afrika Evelyn Opondo amesema yaliyomo kwenye mswada huo yatasaidia kupunguza visa vya mimba za mapema miongoni mwa wasichana.

“Ikiwa tutatoa habari kuhusu masuala ya uavyaji mimba na afya ya uzazi kwa ujumla kwa watoto wetu, tutaweza kupunguza mienendo kama hiyo. Shida ni kwamba tumechukulia masuala ya ngono kama mwiko na hivyo watoto wetu wanakosa ufahamu kuyahusu mapema,” akasema.

Bi Opondo amesema ni kinaya kuwa makanisa ambayo yanamiliki shule za msingi na za upili ndiyo yako katika mstari wa mbele kuhujumu juhudi za serikali za kujumuisha masuala ya afya ya uzazi katika mtaala wa masomo.

“Ni muhimu kwa watoto kupewa elimu ya ngono mapema ili waweze kufanya maamuzi bora wakiwa wakubwa. Na wazazi pia wanafaa kuendelea kutoa elimu hii nyumbani,” akasema Bw Arthur Wekesa ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la Network for Adolescence and Youth of Africa.

You can share this post!

LA LIGA: Sergio Ramos afunga penalti kindumbwendumbwe dhidi...

Nyani Iker Casillas asema ‘tosha gari’ katika...

adminleo