Mtanzania aliyenaswa na Heroin ndani miaka 30 Mombasa
Na BRIAN OCHARO
RAIA wa Tanzania amefungwa jela miaka 30 kwa kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin za thamani ya Sh30 milioni.
Hussein Massoud Eid pia anatakiwa alipe faini ya Sh90 milioni au atumikie kifungo cha ziada cha miaka mitano.
Hakimu Mkuu Mwandamizi wa mahakama ya Mombasa, Edgar Kagoni (pichani), alisema hukumu hiyo itakuwa kama funzo kwa wengine wenye nia ya kujihusisha na ulanguzi wa dawa hizo ambazo zimechangia kuharibu vijana katika ukanda wa Pwani.
“Kwa kuwa mshukiwa hakuwa peke yake katika biashara hii kwani alipatikana akisafirisha dawa hizo, nitamuhukumu kumrekebisha na kuwa funzo kwa wengine ambao watafikiria kufanya kosa kama yake,” alisema hakimu.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya Kiongozi wa Mashtaka Erick Masila kuomba mahakama kumfunga mshukiwa jela maisha na kutozwa faini mara tatu ya thamani ya dawa aliyopatikana nayo.
“Mshukiwa amehukumiwa jela miaka 30, pia, ametozwa faini ya Sh90 milioni au kutumikia miaka mitano zaidi gerezani iwapo atakosa kulipa faini hiyo. Madawa za kulevya alizokamatwa nazo zitaharibiwa na serikali,” Bw Kagoni alisema.
Hakimu huyo alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulithibitisha kuwa mshukiwa alisafirisha dawa hizo kwa kuzihifadhi katika mifuko mieusi.
Aliongezea kuwa upande wa mashtaka ulidhibitisha kuwa Bw Eid ndiye alikuwa katika nyumba ambayo mihadarati hizo zilipatikana na askari wa kupambana na mihadarati.
Pia, Bw Kagoni alisema kuwa ushahidi wa wafanyikazi wa hoteli ambapo mihadarati hizo zilipatikana walidhibitisha kuwa mshukiwa ndiye alikuwa amelipia hiyo nyumba na kwamba alionekana akiingia humo ndani na bagi kubwa ambayo ilibeba hizo mihadarati.
“Nimezingatia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka , ni wzi kuwa mshukiwa alipatikana na mihadarati kwani bagi hiyo ilipatikana kwa nyumba ambalo alikuwa akiishi. Mshukiwa amepatikana na hatia kama alivyoshtakiwa,” Hakimu alisema.
Bw Eid kupitia kwa wakili wake Jared Magolo aliomba mshamaha akisema kuwa hilo lilikuwa kosa lake la kwanza na kwamba amerekebika.
Alisema kuwa amerekebika na kuomba mahakama kumuachilia huru ili aungane na familia yake ambayo ametengana nao kwa miaka mitatu sasa.
“Mshukiwa anjutia kosa lake na angependa kusamehewa na mahakama ili aweze kuendelea na maisha yake ya kawaida. Ana watoto wanne ambao wanamtegemea. Amekaa sana gerezani na tunaomba sifungwe tena akarudi gerezani kwani amerekabika,” Bw Magolo alisema.
“Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi ya usafirishaji wa dawa za kulevya dhidi ya Hamisi na Tinje, kwasababu hiyo, wameachiliwa huru,” Bw Kagoni alisema.
Hakimu huyo aliongezea kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukuwahusisha vilivyo wawili hao na mashtaka dhidi yao hivyo basi hakuwapata na hatia ya kuhusika katika ulanguzi wa mihadarati hizo.
Watatu hao walikuwa wameshtakiwa na kosa la kusafirisha kilogramu 10.022 za heroin ambayo walikuwa wameficha chini ya bagi la kusafiria.
Upande wa Mshtaka ulidai watatu hao walifanya kosa hilo mnamo Machi 16, katika Hoteli ya Regency Park mjini Mombasa.
Wakati wa kukamatwa, polisi walipata dolla 6100, na pesa zingine ambazo zilikuwa katika sarafu ya Madagascar, Tanzania na United Arab Emirates.
Bw Kagoni alitoa amri fedha hizo ziregeshewe Bw Eid kwani hazikutokana na uuzaji wa dawa hizo.