Mtoto afariki katika kisa cha moto Mukuru-Kayaba
Na SAMMY KIMATU
MTOTO wa umri wa miaka tisa alifariki Alhamisi baada ya kuteketea katika kisa cha moto uliotokea katika eneo la Lengo kwenye mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba, kaunti ya Nairobi.
Aidha, nyumba 15 na kilabu ziliteketea kwenye mkasa huo uliowaacha waathiriwa wakikadiria hasara ya mali yenye thamani ya maelfu ya pesa.
Polisi walitambua mwili wa mtoto huyo kuwa wa mvulana kwa jina Ian Kiliku Mutuku.
Fauka ya hayo, Inadaiwa kisa hiki kilitokea mwendo wa saa tatu za asubuhi huku wakazi wengi ambao ni vibarua katika Eneo la Viwanda wakiwa kazini.
Isitoshe, Bi Naomi Kalewa, 43 alikiri alikuwa amelala na mtoto huyo wakati wa kisa kutokea.
“Nilikuwa nimelala lakini nikaamshwa na ukemi kutoka kwa majirani waliokuwa wakiomba usaidizi baada ya moto kuzuka. Nilipotoka nje, nilikumbana na moshi mwingi na ndimi za moto nikashindwa kupumua. Kwa bahati ya Maulana, nilivutwa na kuokolewa na vijana kwa kupandishwa juu ya ukuta wa mawe. Nilichomeka mgongoni sawia na mikononi,” Bi Naomi akaambia Taifa Leo.
Bi Naomi aliongeza kwamba alikuwa akiugua Malaria na kulazwa nyumbani kwa kipindi cha miezi miwili.
Nduru zilieleza kwamba marehemu alikuwa ameachwa kwa Bi Naomi baada ya mamake kwa jina Bi Mutindi aliporauka kwenda kufanya kibarua cha kufua nguo mitaani.
Kando na hayo, mwathiriwa, Bi Elizabeth Mwende, 29 anayemiliki kilabu kilochoteketea alikiri kuwa hakuokoa chochote kutoka kwa baa yake.
“Singeweza kuokoa chochote hata glasi moja wala chupa ya pombe kutokana na moshi ulionitatiza kupumua,” Bi Mwende akasema.
Shahidi, Bw Cosmas Mutiso Kimeu, aliye kadhalika mfanyabiashara karibu na eneo la kisa alisema moto ulianza kutoka kwa nyumba moja kabla ya kusambaa haraka hadi kwa nyumba zingine kufuatia upeo mkali.
Gari la kuzima moto lilishindwa kuingia katika eneo la kisa baada ya kukosa barabara.
Bw Moses Musyoki, 33 aliyekuwa kazini alisema alipoteza kila kitu na kumshukuru Mungu baada ya mkewe aliyejifungua juzi kuokolewa na mwanawe.
Polisi wanachunguza kisa hiki kubaini chanzo cha moto.