Mudavadi adai mabwawa ni njama ya uporaji
WACHIRA MWANGI Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi amedai kwamba miradi ya ujenzi wa mabwawa 57 ni mbinu ya kupora pesa akisema miradi hiyo haiwezi kutekelezwa.
Bw Mudavadi alisema Kenya haina uwezo wa kujenga mabwawa kama hayo na akalaumu wataalamu wa sekta mbali mbali nchini kwa kushindwa kupigana na ufisadi.
Alisema ni wao wanaoidhinisha miradi hewa ambayo inatumiwa kupora mabilioni ya pesa na kwa kufanya hivyo wanachangia katika ufisadi.
“Hakuna serikali nyingine popote duniani ambayo imewahi kuahidi kujenga mabwawa 57 wakati wa uongozi wake. Ikiwa China haiwezi kuahidi hivyo, ama Amerika, ama Saudi Arabia yenye ukwasi wa mafuta, sisi ni nani?” aliuliza alipofunga kongamano la wataalamu mjini Mombasa.
Alisema hiyo ni mbinu ya maafisa wakuu serikalini kupora rasilimali za umma. Alisema Kenya imetumia takriban Sh165 bilioni kwa ujenzi wa mabwawa kwa miaka sita iliyopita, japo hakuna hata moja limekamilika. Serikali imesema inanuia kujenga mabwawa hayo miongoni mwa miradi mingine ili kuinua maisha ya Wakenya.
“Kumekuwa na tofauti kubwa sana kuhusu gharama na kiwango cha fidia ambacho hakieleweki. Wakati mwingine, huduma sawa zimetolewa zaidi ya mara moja na zote kulipiwa,” akasema.
Aliwakosoa wataalam ambao wamekuwa wakihusika katika hatua tofauti kuwa pia walichangia katika ufisadi, ambao unazidi kulizorotesha taifa.
Kiongozi wa chama cha ANC aliwahimiza wataalam katika sekta mbalimbali serikalini kufanya kazi zao inavyofaa na kushirikiana kumaliza ufisadi ambao unaelekea kumaliza taifa, akisema wakiruhusu siasa kuingilia kazi zao mustakabali wa taifa utakuwa gizani.
“Masuala yaliyo mbele yetu kama nchi ni mazito hivi kwamba yanahitaji wataalam kuwa makini na wasijihusishe na siasa. Kadri muda unavyosonga, inakuwa wazi kuwa suluhu za changamoto nyingi tunazokumbana nazo zitapatikana kwa wataalam,” akasema Bw Mudavadi.
Kiongozi huyo alikuwa akizungumza katika kongamano la wataalam katika hoteli ya Pride Inn, eneo la Shanzu, Kaunti ya Mombasa. Aliwataka wataalamu hao kusaidia kuangamiza ufisadi nchini.
Alisema taifa liko katika njia panda na kuongeza: “Sharti tuamue ikiwa kama taifa tunataka kuisha ama kuendelea kuishi. Chaguo tutakalofanya litakuwa na matokeo mazito kwetu kama wataalam.”
Matamshi ya kiongozi huyo yalikuja wakati madai ya ufisadi kwenye ujenzi wa mabwawa yameshika moto nchini na kusababisha wanasiasa kulaumiana,hasa kuhusu madai kuwa Sh21 bilioni ziliporwa katika miradi ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror.
Uchunguzi kuhusu pesa hizo umezua mjadala mkali kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga. Bw Ruto amekuwa akidai uchunguzi umeingizwa siasa na akapendekeza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti afutwe.
Anasisitiza kuwa ni Sh7.8 bilioni zilizolipwa na hazikupotea inavyodaiwa. Bw Mudavadi aliwataka wataalamu kusaidia ili taifa lisiporomoshwe na ufisadi. “Sharti tujiulize ni wapi wataalam wamechangia katika kuliangusha taifa, wataalam wanafaa kufanya nini?
Na taifa likiendelea na mwelekeo huu, wataalam watakuwa na maana tena?” kiongozi huyo akauliza.