Habari Mseto

Mudavadi na Weta watakiwa kuingia serikalini

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SHABAN MAKOKHA

WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Kakamega wamewarai vigogo wa siasa za eneo la Magharibi, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kuiga mfano wa vinara wa vyama vya ODM na Wiper na kujiunga na serikali.

Mbunge wa Lurambi Titus Khamala na mwenzake wa Navakholo Emmanuel Wangwe wamesema kwamba inasikitisha viongozi hao wanaendelea kusalia kwenye baridi kisiasa badala ya kufanya kazi pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Wangwe alitoa mfano wa Bw Musyoka aliyeamua kushirikiana na Rais ijapokuwa aliwachwa nje na Bw Odinga katika mkataba wake wa makubaliano na Rais Kenyatta na kusema kwamba iwapo Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula watajiunga na serikali wataimarisha uwezo wa jamii ya Waluhyia kutoa mwaniaji wa urais mwaka wa 2022.

Kwa upande wake Bw Khamala alifichua kwamba Bw Musalia atapata wadhifa muhimu katika Muungano wa Afrika Mashariki jinsi Bw Odinga alivyoteuliwa kama Mwakilishi wa bara Afrika katika maswala ya miundombinu.

“Nina uhakika hata Bw Wetang’ula atapata kazi katika muungano wa kiuchumi wa kaunti ya ziwa Viktoria,” akaongeza Bw Khamala akihutubu wakati wa ibada katika Dayosisi ya kanisa la kianglikana, Milimani mjini Kakamega siku ya Jumapili.

Hata hivyo Bw Mudavadi amekuwa akishikilia kwamba hawezi kushirikiana na utawala wa Rais Kenyatta kwa sababu chama cha Jubilee ni washindani wake na kinajitayarisha kuutetea wadhifa wa urais mwaka wa 2022.