Muite aomba korti itupe ombi la KRA kupima fatalaiza
Na RICHARD MUNGUTI
KAMPUNI iliyoagiza fatalaiza inayodaiwa kuwa na madini ya zebaki (mercury) pamoja na washukiwa wengine 11 Jumatatu waliomba mahakama kuu itupilie mbali ombi la Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) la kutaka agizo la kuamriwa maafisa wake wafike kortini isitishwe.
Wakili Paul Muite aliyeongoza mawakili Ken Nyauncho na Edward Oonge kupinga hatua hiyo ya KRA walimweleza Jaji Pauline Nyamweya kuwa “KRA imekaidi agizo la mahakama mara nne na haipasi kuruhusiwa kuendelea na kuvunja sheria.”
Bw Muite alimweleza Jaji Nyamweya kwamba KRA imekaidi mara mbili maagizo ya Jaji Daniel Ogembo ifadhili kupimwa tena kwa mbolea iliyoingizwa nchini Novemba 2017 kubaini ikiwa ikon a Zebaki.
Aliongeza kusema KRA imekaidi mara mbili tena agizo la hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot ifadhili upimwaji wa mbolea hiyo katika maabara ya kibinafsi.
Jaji Nyamweya alimwuliza wakili George Ochieng iwapo KRA imewahi fika mbele ya Cheruiyot na kuwasilisha malalamishi yake.
“Je, unataka hii mahakama itoe maagizo ya aina gani iwapo haujafika mbele ya hakimu mwandamizi Cheruiyot?” Jaji Nyamweya akauliza.
“Utatumia Kifungu 165 cha katiba kinachoipa mahakama mamlaka ya kusimamia mahakama za mahakimu kutekeleza sheria ipasavyo,” akajibu Ochieng.
Mahakama ilimwuliza, “Unataka hii mahakama ifanyie nini KRA maanake imekaidi agizo la hii mahakama mara mbili?” Jaji Nyamweya.
“Naomba tu hii mahakama itumie uwezo wake na kuwazuia maafisa wawili wa KRA na mamlaka ya bandari kutofika mahakamani,” Ochieng.
Wakili huyo alisema mkurugenzi mkuu mwandamizi wa shirika la ukadiriaji wa ubora wa bidhaa (Kebs) Bernard Nguyo alifika mbele ya Bw Cheruiyot na kueleza ugumu wa kutekelezwa kwa maagizo hayo.
Lakini hakimu alimwamuru Bw Nguyo aamuru maafisa wa Kebs wanaohusika na ubora wa bidhaa za kutoka ng’ambo wapime mbolea hiyo.
Bw Nyauncho alimweleza jaji huyo KRA ni kibaraka wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ambaye alikaidi maagizo hayo na sasa anatumia KRA kuvuruga maagizo ya mahakama.
Mahakama ilielezwa hakuna gharama ama hasara ambayo KRA itapata kwa kufungua mabohari yanayohifadhiwa mbolea hiyo na sampuli kuchukuliwa na kupimwa katika maabara ya kibinafsi kubaini ikiwa mbolea hiyo tani 3000 ilyoingizwa nchini na kampuni ya OCP (K) Limited iko na madini ya Zebaki.