Habari Mseto

Mung’aro aangukia mamilioni ya NGO kusaidia kupaisha sekta ya samaki

Na MAUREEN ONGALA August 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Kilifi inaangazia uwekezaji mkubwa katika sekta ya ufugaji wa samaki ili kuimarisha uzalishaji chakula cha kutosha na kubuni nafasi za ajira kwa vijana na makundi mengine yaliyotengwa katika jamii.

Gavana Gideon Mung’aro alisema shirika lisilo la kiserikali la Farm Africa limetenga dola milioni tatu (Sh387 milioni) kwa ajili ya ruzuku na dola milioni 5 (Sh645 milioni) kwa ajili ya mikopo kwa miradi ya ufugaji wa samaki.

Kulingana naye, hatua hiyo itasaidia kustawisha sekta ya uvuvi ambayo bado inatatizika katika uzalishaji.

Mkuu huyo wa kaunti alisema ufadhili huu utawasaidia sana wenyeji kwa sababu wengi wao bado wanatumia njia za jadi za uvuvi ambazo hazina ufanisi.

“Ufugaji wa samaki ni mradi ambao unaweza kufanya vyema Kilifi kwa sababu ndiyo kaunti pekee yenye ufuo mrefu zaidi katika kaunti zote sita za Pwani, na kwa hivyo tuna nafasi ya kutosha kwa mabwawa mengi ya samaki baharini,” alisema.

Alikuwa akizungumza Jumatatu alipotia saini Mkataba wa Makubaliano (MOU) na mashirika mawili kuhusu masuala ya sekta ya kilimo.

Utiaji saini huo ni sehemu ya juhudi za kuwavutia wawekezaji zaidi kabla ya Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kilifi (KIIC) mwezi Novemba mwaka huu.

Alisema analenga kuleta wawekezaji wengi iwezekanavyo katika kaunti hivyo kabla ya hafla itakayofanywa Vipingo.

Maelewano kati ya Serikali ya Kaunti na Farm Africa yapo kwenye mpango wa miaka mitano wa Vijana katika Ufugaji Endelevu wa Majini (YISA) unaofadhiliwa na Wakfu wa Master Card unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake 150,000 na watu wanaoishi na ulemavu kupata ujuzi wa ufugaji wa samaki, masoko, na kubuni nafasi za ajira.

Mkurugenzi wa shirika la Farm Africa, Bi Mary Nyale, alisema vijana wengi hawana ujuzi wa ufugaji wa samaki licha ya sekta hiyo kuwa na uwezo wa kuwainua kimaisha.

“Vijana wengi hawajui fursa iliyopo ndani ya sekta ya ufugaji wa samaki au hawana ujuzi na maarifa muhimu ya kujihusisha kikamilifu. Mipango ya mafunzo na mipango ya elimu ni muhimu ili kuziba pengo hilo,” alisema.

Bi Nyale aliongeza kuwa, shirika hilo linatumia mbinu zote kuwawezesha vijana na kwamba pamoja na washirika wengine watekelezaji kuandaa mtaala kuhusu Ufugaji wa samaki na utamaduni wa Mari utakaofunzwa katika taasisi za TVET mjini Kilifi.

Alibainisha kuwa, upatikanaji mdogo wa rasilimali ni changamoto kwa vijana wajasiriamali, inayozuia uwezo wao wa kuanzisha au kupanua shughuli za ufugaji wa samaki.

Makubaliano mengine kati ya kaunti na kampuni ya Bear Machines Afrika Mashariki ni kuhusu kilimo cha kakao kwa lengo la kuzalisha tani 1.5 za kakao kwa kila ekari 30 kila mwaka.

Afisa wa Masoko Martin Mugwanja alisema Bear Machines Afrika Mashariki itaingiza mtaji wa zaidi ya dola milioni 162 katika mradi huo wa miaka miwili.

Mradi utaanza kwa kuanzisha shamba la mfano la kakao na kuwashirikisha wakulima wanaopakana na eneo hilo.