Habari Mseto

Mungiki wazimwe kabisa Mlima Kenya – Kibicho

May 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA GEORGE MUNENE

KATIBU katika Wizara ya Usalama wa Ndani Bw Karanja Kibicho ameamuru kuzimwa kwa kundi la uhalifu la Mungiki linalohangaisha wafanyabiashara eneo la Mlima Kenya.

Amewaamuru washirikishi wa kaunti za eneo hilo kushirikiana na polisi kuondoa wahuni hao kwa jamii haraka iwezekanavyo.

“Mungiki wamerudi na wanasababisha hofu kwa wanabiashara, wanapaswa kukabiliwa vilivyo,” alisema Jumatano eneo la Ngurubani, Kaunti ya Kirinyanga akiwa kwenye ziara ya miradi ya maendeleo.

Alisema kwamba Mungiki wanazunguka wakidai pesa ya kuwalinda wafanyabiashara ambao wanapitia wakati mgumu wakati huu wa corona.

Bw Kibicho alisisitiza kwamba Mungiki wamejaa Kirinyanga ambapo wanakusanya pesa kwa wafanyabiashara kinyume cha sheria.

“Mungiki ni hatari na wanapaswa kukabilianwa bila huruma. Shughuli zao za kihahilfu hazitakubalika Mlima Kenya ama mahali popote humu nchini,” alisema.

Wanabiashara wamekuwa wakiteta kwamba Mungiki wamerudi na kwamba wanawazuia kufanya biashara kwa amani, huku wakiwapunguzia faida.

Bw Kibicho alisema kwamba inasitikisha kwamba wanabiashara wanaong’ang’ana kupata riziki ya kila siku wanazipoteza pesa zai kwa wahalifu wazembe wanaopenda kuvuna wasipopanda.

Wakati huo huo afisa huyo alionya polisi na wasimamizi wanaowatetea wenye vilabu wanaofungua baa kinyume na mikakati iliyowekwa ya vilabu na maeneo ya burudani kubakia kufungwa.