Habari MsetoSiasa

Murathe: 'Timu Tangatanga' ikome kuzua uongo dhidi ya Ruto

August 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WAMBUI

NAIBU kiongozi wa Jubilee David Murathe Jumapili aliwataka baadhi ya wafuasi sugu wa Naibu Rais William ruto wakomeshe madai ya kuwepo njama ya kumharibia naibu huyo kuchukua uongozi mwaka 2022.

Kiongozi wa Wengi katika bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen ambaye amejitangaza kuwa mwanachama wa kundi la Tanga Tanga, amedai kwenye mikutano kadhaa kwamba baadhi ya watu katika ikulu wanaendeleza njama ya kuhakikisha kuwa Bw Ruto haingii uongozini.

Lakini Jumapili akizungumza wakati wa ibada katika Kanisa la AIC Theta lililoko Gatundu Kusini, Bw Murathe alisema wanachama hao wa kundi hilo la TangaTanga ndio wanaomharibia Bw Ruto.

“Ningependa kumwambia Moses (Kuria) na wenzake wa kundi linalojiita Tanga Tanga kwamba ni wao wanaomharibia Naibu Rais kwa sababu Katiba inasema mshindi atapata asilimia 50+1. Unajuaje kwamba hiyo kura moja ndiyo ambayo unaipoteza kwa matamshi ya kumzulia Rais?”akauliza.

Bw Murathe alitaka wanasiasa wa mrengo wa bw Ruto wasema hadharani ni wakati gani ambapo Rais Kenyatta alitangaza kuwa hamuungi tena Bw Ruto.

“Si rais mwenyewe alisema kuwa muhula wake ukiisha ni naibu wake atakayemrithi? Alisema lini au wapi kwamba amebadili msimamo huo? Acheni huu uzushi mnaozunguka kila mahali mkiueneza bila ya haya,” akasema.

Kiongozi huyo wa chama kadhalika alionya kuwa Jubilee haitasita kuwachukulia hatua watu wanaotoa matamshi au kufanya vitendo ambavyo vinahatarisha umoja wa chama hicho.

Aliungwa mkono na mbunge wa Cherangany, Bw Joshua Kuttuny, alisema viongozi wanapaswa kufahamu kuwa wako katika serikali moja.