Murkomen na Kutuny wapakana tope mitandaoni
NA PETER MBURU
Wanasiasa kutoka North Rift Kipchumba Murkomen na Joshua Kutuny wamezidi kupakana matope kwenye mitandao ya kijamii, wakivutia umakinifu wa Wakenya wanaporushiana maneno.
Ubishi ulianza wakati wawili hao walikuwa katika mahojiano ya pamoja na mwanahabari wa Citizen TV Jeff Koinange, wakati Bw Kuttuny (Mbunge wa Cherangany) alidai kuwa alimwokoa Bw Murkomen (seneta wa Elgeyo Marakwet) kutoka kwa umaskini na kumfanya seneta.
Lakini viongozi hao walionekana kutoridhika na mavamizi kwenye runinga kwani Jumatano na Alhamisi waliendelea kushambuliana, Wakenya waliovutiwa nao wakiingilia mjadala huo ulioonekana kuibua uchangamfu.
Katika makabiliano hayo, Wakenya wengi walionekana kufurahishwa na matamshi ya Bw Kutuny ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akimkosoa naibu wa Rais William Ruto, wengi wakimtaka kukubali kuwa alisaidiwa na Bw Kuttuny.
Wakati wa mahojiano hayo, Bw Kutuny alikuwa amemwambia seneta Murkomen “Nilikuinua kutoka mitaani na kukufanya seneta, nilikuwa nakupa pesa kila wiki, mke wangu alikuwa anakupa pesa kila wiki na hata rekodi za MPESA bado ziko.”
Bw Kutuny alichapisha kanda ya mahojiano hayo ambapo alikuwa akisema hivyo kwenye akaunti yake ya Facebook Jumatano, akimchochea Bw Murkomen kulipiza kisasi Alhamisi.
“Wale watu walinitumia pesa kwa Mpesa zaidi ya miaka 10 iliyopita kupitia wake zenu nab ado mmehifadhi rekodi hadi leo tukutane pale java saa kumi jioni tunywe kahawa,” akasema seneta huyo.
Majibizano hayo yalivutia mchango wa Wakenya mitandaoni kwa wingi.
“Kutuny alikuwa mwokozi wako, heshimu hilo rafiki yangu, rekodi za mpesa zinaweza kutolewa,” akasema Hempstone Ongidi.
Fredrick Matengo naye alisema “Nilidhani wewe ni mkristo, Kutuny alikufaa ulipokuwa katika shida. Unaweza kuwa na pesa sasa lakini wakati huo hukuwa nazo, unafaa kushukuru.”
Lakini ujumbe huo ulionekana kumkera Bw Murkomen ambaye alijibu, “Akanisaidia??? Yani unaamini huo upuuzi?”
“Naelekea kuamini kwa kuwa aliposema ulipandwa na hasira,” akasema Kirui Luke.
Wengine walichapisha picha walizodai ni za seneta Murkomen alipokuwa masikini, ili kudhihirisha kuwa kweli mwanzo wake haukuwa wa kuvutia.
Lakini kwenye ukurasa wa Bw Kutuny, Wakenya walishangaa ukweli wa madai yake, kwani wengi walidai kuwa Bw Murkomen alikuwa mhadhiri kabla ya kuchaguliwa kuwa seneta.
“Nilidhani kabla ya kuingia katika siasa OKM alikuwa mhadhiri,” akashangaa Eric Tanui.