• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 12:36 PM
Mutua asisitiza alimwangusha Wavinya uchaguzini

Mutua asisitiza alimwangusha Wavinya uchaguzini

Na SAM KIPLAGAT

GAVANA wa Machakos Dkt Alfred Mutua amesisitiza kuwa alishinda kiti cha ugavana kwa njia ya haki na akakosoa Mahakama ya Rufaa kwa kubatilisha ushindi wake kwa sababu ya hitilafu ndogo za kiufundi.

Kupitia wakili wake Kioko Kilukumi, Dkt Mutua aliambia Mahakama ya Juu kwamba, afisa wa uchaguzi alitumia karatasi tofauti kujumuisha na kutangaza matokeo badala ya fomu rasmi.

Alitaja hatua hiyo kama mabadiliko madogo ambayo hayawezi kufanya ushindi wake kubatilishwa akisema haiwezi kufanya matokeo hayo kutothibitishwa.

“Mahakama haikupata kuwa matokeo yalikuwa na makosa au kuongezwa au ya kubuni kwa njia yoyote. Fomu zote zilitiwa saini na maajenti wa Wiper miongoni mwa watu wengine,” alisema Bw

Kilukumi.

Wakili huyo alisema kutiwa sahihi kwa fomu hizo huwa sio zoezi lisilo na maana na kuongeza kuwa, msimamizi wa uchaguzi alitumia karatasi inayotambuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Alimweleza Jaji Mkuu David Maraga na majaji Mohamed Ibrahim, J.B. Ojwang, Njoki Ndung’u na Isaac Lenoala kufutilia mbali uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ambao ulibatilisha ushindi wa Mutua.

Dkt Mutua amelaumu majaji William Ouko, Mohamed Warsame na Gatembu Kairu, akisema walikosea kisheria kwa kutumia sehemu za katiba visivyo na kufanya wafikie uamuzi usiofaa.

Kwa upande wake, Bi Wavinya Ndeti alisema hakuna anayejua aliyeshinda kiti cha ugavana cha Machakos kwa sababu matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi hayawezi kuthibitishwa.

Kupitia wakili Ahmednasir Abdullahi, Bi Ndeti alisema matokeo yaliyotangazwa Agosti 11 mwaka jana yalikuwa feki, yalikuwa ya kubuniwa na hakuna njia ambayo yanaweza kuthibitishwa.

Kulingana na Bi Ndeti, kwa vile afisa wa uchaguzi alikosa kutumia fomu inayotambuliwa kisheria, uhalali wa matokeo hauwezi kuthibitishwa.

“Suala la jinsi matokeo yanafaa kuthibitishwa liliamuliwa katika kesi ya Raila Odinga 2017. Mfumo unaotumiwa unafaa kuwa rahisi, wazi na unaoweza kuthibitika. Kukosa kuthibitishwa ni suala lenye uzito kikatiba,” alisema Bw Abdullilahi.

Kwenye uchaguzi wa Agosti 8 mwaka jana, Dkt Mutua wa chama cha Maendeleo Chap Chap alipata kura 249,603 dhidi ya 209,141 za Bi Ndeti.

Jaji wa Mahakama Kuu Aggrey Muchelule alitupilia mbali kesi ya Bi Ndeti ambapo alipinga ushindi wa Dkt Mutua.

Hata hivyo, Bi Ndeti alikata rufaa na majaji watatu wakabatilisha ushindi wa Dkt Mutua wakisema msimamizi wa uchaguzi alitumia fomu isiyofaa kutangaza matokeo.

Dkt Mutua hakuridhika na akawasilisha kesi katika Mahakama ya Juu iliyozuia kiti chake kutangazwa wazi hadi kesi yake iamuliwe.

Jana, majaji wa Mahakama ya Juu walisema watafahamisha pande zote kuhusu uamuzi wao.

You can share this post!

Ndani kwa kumbaka na kumwambukiza mpwa HIV

Nyuki wavamia kijiji na kuua mwanamke na kondoo wake

adminleo