Habari MsetoSiasa

Mutua atimua maafisa 30 wazembe sababu ya ufisadi

September 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Peter Mburu

Gavana wa Machakos Alfred Mutua jana aliwatuma kwenye likizo ya lazima maafisa 30 wa kaunti hiyo jana, kufuatia visa vya ufisadi na kutofanya kazi ipasavyo kwenye sekta ya ujenzi na kutaka maafisa husika wafanyiwe ukaguzi wa maisha yao kubaini ikiwa wameiba mali ya umma.

Gavana huyo alisema kulikuwa na visa vikuu vya ufisadi kaunti hiyo, haswa katika sekta ya ujenzi kwenye idara za utoaji leseni za kuruhusu ujenzi kuanza, eneo la Mavoko.

Alisema uchunguzi wa awali wa serikali ya kaunti ulibaini kuwa maafisa husika walipunguza bei ya huduma za kutoa ramani za ujenzi, vyeti vya kazi, wakashirikiana na wanyakuzi wa ardhi kuhalalisha umiliki wao wa mashamba bila kuwa na vyeti vinavyohitajika na kupokea hongo.

“Ninachukua fursa hii kurekebisha visa vikuu vya ufisadi kaunti hii katika afisi zinazotoa huduma za leseni za ujenzi. Nina furaha kuwa idara ra upelelezi (DCI) tayari imetuma maafisa wake kuanza uchunguzi, huku tukisubiri idara zingine za upelelezi kujiunga nasi siku zijazo,” akasema Gavana Mutua.

Alisema hali ya ufisadi kaunti hiyo vimesababisha serikali kupoteza pesa nyingi, licha ya kusababisha ukosefu mkubwa wa kazi miongoni mwa vijana.

Alielekeza maafisa hao kuwasilisha vyeti kadhaa vikiwemo akaunti zao na za wake au waume zao za benki ili zikaguliwe Jumatatu asubuhi.