Mvua yazua maafa Pwani
Na WAANDISHI WETU
MTU mmoja alifariki Alhamisi baada ya kusombwa na mafuriko katika eneo la Kadzandani, eneo la Kisauni katika Kaunti ya Mombasa.
Mamia ya familia nazo ziliachwa bila makao kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha Pwani.
Tayari familia kadha zimeanza kuhamia nyanda za juu baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jumatano usiku.
“Nimelazimika kuhamia kwa jirani baada ya nyumba yangu kufurika. Mvua ilianza kunyesha saa moja usiku na kuendelea mfululizo usiku kucha. Tumeingia hofu,” alisema mkazi John Charo.
Mji wa Mombasa na viunga vyake ulikuwa umefurika jana kutokana na mvu ya usiku kucha.
Biashara ziliathirika huku ofisi zikifunguliwa zikiwa zimechelewa baada ya wafanyakazi kukosa kufoika kazini kwa wakati.
Hali ilikuwa ngumu hata zaidi kwa wakazi wa maeneo ya Utange na Kadzandani, ambako barabara zilifunikwa kabisa na maji.
“Nimejaribu kubeba wateja lakini mvua imenyesha kweli. Nimelazimika kurejesha pikipiki yangu nyumbani hadi hali itulie,” alieleza Bw Juma.
Barabara inayounganisha shule mbili za msingi eneo la Majaoni na Shanzu pia zilikuwa hazipitiki na kuzuia shughuli za masomo kuendelea.
“Barabara kati ya Nyemuteka na Fumathoka imejaa maji na watu hawawezi kuipitia,” alisema mkazi wa Majaoni, Costance Kanze.
Eneo kati ya muungano wa Kiembeni na kituo cha kibiashara cha Wema, Bamburi, pia lilifurika na kuzima usafiri wa matatu zinazotumia barabara ya Bamburi-Utange.
Mvua hiyo imeweka wazi hali mbovu ya kivuko cha Likoni kinachounganisha Kenya na Tanzania.
Hali mbovu ya mabomba ya kupitisha maji taka katika kaunti ndogo ya Likoni ilisababisha mafuriko kujaa katika kivuko hicho na kuzuia abiria kufikia kwenye feri.
Kulingana na tahadhari iliyotolewa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa siku ya Jumatano, mvua kubwa ilitarajiwa kunyesha kuanzia jana hadi kesho katika ukanda mzima wa Pwani.
Taarifa ya Antony Kitimo, Winnie Atieno, Ahmed Mohamed na Samuel Baya