Habari Mseto

Mvurya ausifu mpango wa elimu katika kaunti

October 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya amesifu uongozi wake akisema serikali yake imewekeza katika sekta ya elimu.

Bw Mvurya amewataka wazazi kuhakikisha wanafunzi wote wanatilia maanani elimu.

“Mradi wetu wa ‘Elimu ni Sasa’ unasaidia kufanikisha elimu kwa zaidi ya wanafunzi 4,800 kwenda masomo ya bure shule za sekondari za kitaifa. Wengine zaidi ya 2,000 wakaenda vyuo vikuu huku zaidi ya 50,000 wakipata nafasi katika shule za kaunti,” alisema Bw Mvurya.

Akiongea alipotoa hundi ya Sh3.1 milioni kwa sekta ya elimu kusaidia wanafunzi 84 wa vyuo vikuu, Bw Mvurya alisema serikali yake pia imejenga shule zaidi ya 469 za chekechea na kuajiri walimu 700.

“Hao ni walimu ambao wameajiriwa kudumu hadi watakapostaafu. Kwa sasa tunajenga taasisi ya mafunzo wa ualimu ili kuhakikisha tunaboresha sekta ya elimu,” alisisitiza Bw Mvurya.

Gavana huyo aliwataka wanafunzi kutia bidii masomoni na kuafikia malengo yao.