Mwalimu wa dini jela maisha baada ya mahakama kumpata na kosa la wizi wa mabavu
Na KALUME KAZUNGU
MWALIMU wa dini ya Kiislamu amehukumiwa kifungo cha maisha baada ya mahakama ya Lamu kumpata na kosa la wizi wa mabavu.
Ustadhi Abdulrahman Mohamed Bwanaheri, 62, ambaye pia ni baba wa watoto wanane, alikutwa na kosa la wizi huo wa mabavu na hata kutumia silaha hatari – upanga – ambapo alimkata na kuhatarisha maisha ya Bi Mwanaisha Bakuri Saburi wakati akitekeleza wizi huo.
Mahakama imefahamishwa kwamba mnamo Machi 12, 2018, Bwanaheri alimvamia Bi Mwanaisha Bakuri Saburi, karibu na msikiti wa Anisa ulioko kisiwani Lamu majira ya saa tatu asubuhi, ambapo aliiba mkoba wake wenye pesa taslimu Sh60,000 mali yote aliyoiba ikiwa jumla ya Sh125,500.
Mahakama pia ilijulishwa na ikathibitisha kwamba Bwanaheri alitumia silaha hatari ya upanga na pia nguvu wakati alikuwa akitekeleza wizi huo wa mabavu.
Wakati wa kisa hicho, Bi Saburi aliachwa na majeraha mabaya ya upanga kichwani na mikononi.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba, amesema ni kinyume cha sheria hasa kifungu cha 295 kinachosaidiwa na ibara ya 296(2) kuhusu wizi wa mabavu na kwamba yeyote anayepatikana na hatia hustahili kupata adhabu kali, ikiwemo ile ya kifo.
Bw Temba alisema jumla ya mashahidi watano walifika kortini kutoa ushahidi wao kuhusiana na kesi hiyo, hivyo kumpata Ustadhi Bwanaheri kwamba alihusika katika kutekeleza wizi huo wa mabavu na hata kuhatarisha maisha ya mlalamishi.
“Umepatikana na hatia ya wizi wa mabavu kinyume cha sheria, kifungu nambari 295 kinachoendana pamoja na 296 (2). Hivyo mahakama inakupa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani. Una siku 14 za kukata rufaa,” akasema Bw Temba.
Amuachia Mungu
Akitoa kauli yake baada ya uamuzi kutolewa, Bwanaheri ameshikilia kuwa yote yaliyoamuliwa “ni maonevu” lakini akasisitiza kuwa yote anamuachia Mungu.
“Nashukuru kwa yote yaliyotendeka. Mimi bado nitashikilia kuwa kesi hii ni ya kuonewa tu lakini yote ninamuachia Mungu muweza wa yote. Niko tayari kutumikia kifungo hiki cha maisha lakini Mungu ndiye atakayenilipia. Sitaacha kumuomba yeye,” akasema Bwanaheri akiwa kizimbani.
Aidha kulikuwa na kilio kwa upande wa wanafamilia wa mhukumiwa ambao walikuwa kortini wakifuatilia kesi hiyo kuanzia mwanzo hadi kipindi hukumu inatolewa.
Polisi walikuwa na wakati mgumu kuwatenganisha wanafamilia hao na mhukumiwa, ambapo wengi walirudi nyumbani huku wakibubujikwa na machozi ya majonzi kufuatia kifungo cha maisha alichopewa kiongozi huyo wa dini.