Habari Mseto

Mwanafunzi afadhiliwa baada ya masaibu yake kuangaziwa na ‘Taifa Leo’

December 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na OSBORN MANYENGO

MTAHINIWA aliyeibuka bora zaidi katika shule ya umma ya Kaptien, Kaunti ya Trans-Nzoia kwa kuzoa alama 406 katika mtihani wa KCPE mwaka huu na kuteuliwa kujiunga na shule ya Kitaifa ya Kapsabet Boys hatimaye amepata ufadhili.

Gazeti la Taifa Leo lilikuwa limeangazia masaibu ya mwanafunzi huyo ambaye mustakabali wake kimasomo ulikuwa umetiliwa shaka.

Ochieng Michael Destiny, 15, amepata ufadhili wa miaka minne kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Trans-Nzoia.

Ochieng na mzazi wake walikuwa na furaha isiyo na kifani baada ya kukutana na gavana wa Trans-Nzoia, Patrick Khaemba ambaye alimhakikishia atamlipia karo ya miaka minne na kumnunulia sare za shule na vitabu.

“Nilipoambiwa na babangu kuwa baada ya kuangaziwa na Taifa Leo, afisi ya gavana iliwasiliana naye na kumhakikishiakuwa nitapata ufadhili wa masomo sikuamini. Nashukuru Taifa Leo kwa kuniangazia na pia Gavana wetu kuhakikisha nimeendelea na masomo yangu ya upili,” akasema Ochieng.

Mwanafunzi huyo alivunja rekodi kwa kuibuka mwanafunzi wa kwanza kupata alama zaidi ya 406 tangu shule hiyo ianzishwe zaidi ya miaka ishirini iliyopita. Aliyemfuata alipata alama 304.

Alisifiwa kuwa kijana mwenye bidii ambaye ni kifungua mimba katika familia yao. Ndoto yake ni kuwa daktari baada ya kumaliza masomo yake ya juu.