Mwanafunzi wa chuo azuiliwa siku 21 kwa mauaji ya mpenzi wake
POLISI wameruhusiwa kumzuilia kwa siku 21 mwanafunzi wa chuo kikuu cha Multi-Media (MMU) kwa mauaji ya mpenzi wake.
Hakimu mwandamizi mahakama ya Kibra Zainab Abdul aliamuru Erick Mutinda Philip mwenye umri wa miaka 19 azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Aprili 28, 2025.
Bi Abdul alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umama (DPP) Renson Ingonga ataamua ikiwa Mutinda atafunguliwa shtaka la mauaji ya mpenzi wake anayejulikana kama Sylvia Kemunto.
Wote wawili; Sylvia na Mutinda walikuwa wanafunzi MMU.
Hakimu alikubalia ombi la afisa anayechunguza kesi hiyo kwamba anahitaji muda wa kukamilisha uchunguzi na kuandika taarifa za mashahidi.
Mahakama ilifahamishwa uchunguzi wa DNA unahitaji kufanywa kabla ya shtaka kufunguliwa.
Hakimu aliambiwa sampuli za damu kutoka kwa nguo na vifaa vilivyopatikana vinahitaji kufanyiwa ukaguzi wa kimaabara kubaini ikiwa zitamlenga mshukiwa huyu.
Pia, mchunguzi wa kesi hiyo alieleza korti kuwa upasuaji wa maiti haujafanywa kubaini kilichosababisha kifo cha Sylvia.
Wakili wa familia ya marehemu, Bw Danstan Omari alieleza mahakama kwamba suala ambalo polisi wanachunguza ni mauaji ya wanawake kiholela.
“Naomba hii mahakama ikubalie polisi wamzuilie Mutinda kwa vile uchunguzi huu na matokeo yake yatakuwa funzo kwa wanaume wanaoua wanawake kiholela. Hii mahakama inahitaji kulinda na kutetea haki za wasichana na wanawake kwa jumla,” Bw Omari alisema.
Hata hivyo, wakili anayemwakilisha Mutinda aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “mshukiwa alijisalamisha kwa polisi.”
Hakimu alielezwa Mutinda ameahidi kushirikiana na polisi wakati wa uchunguzi uliosalia.
“Mshukiwa huyu hana hata pasipoti na kamwe hatatoroka hata akiachiliwa kwa dhamana,” Bi Abdul alifahamishwa.
“Baada ya kutathmini mawasilisho ya upande wa mashtaka ni bayana uchunguzi haujakamilishwa. Polisi wanahitaji muda kukamilisha mahojiano,” Bi Abdul alisema huku akiamuru mshtakiwa azuiliwe kwa siku 21.