Mwanahabari wa Standard kulipwa Sh9m kwa kuchafuliwa jina
Na MAUREEN KAKAH
UAMUZI wa mahakama ambapo wanawake wawili waliagizwa kumlipa fidia mwanahabari mmoja Sh9 milioni huenda ukazua maswali kuhusu utumizi wa mitandao kumharibia mtu sifa.
Hakimu Mkuu Addah Obura aliwaagiza Prof Wambui Mwangi na Bi Shajia Patel kumlipa mwanahabari Tony Mochama wa Standard Media Group fedha hizo kwa kuchapisha jumbe za kumharibia sifa katika mitandao ya kijamii.
Wawili hao waliandika jumbe hizo kumhusu miaka mitano iliyopita.
“Kuna thibitisho la kutosha jumbe hizo zilimharibia sifa Bw Mochama, hivyo anastahili kulipwa. Ninawaagiza washtakiwa kumlipa kiasi cha Sh8 milioni kwa kuharibiwa sifa na Sh1 milioni zaidi kama adhabu kwao,” akaagiza hakimu.
Bw Mochama, anayefahamika kama ‘Smitta’ aliwashtaki wawili hao baada yao kudai alimdhulumu mmoja wao kimapenzi mnamo Septemba 2014.
Prof Mwangi aliandika jumbe kadhaa katika mtandao wa Twitter, akishangaa ni kwa nini mwanahabari amdhulumu kimapenzi mwanamke na ikiwa kuna sheria yoyote iliyotoa taratibu maalum kuhusu adhabu ya kitendo hicho katika shirika alilofanyia kazi.
Kando na hayo, aliwaomba wafadhili wa masomo ya Bw Mochama, wahisani na mwajiri wake kutathmini uzito wa madai hayo.
Vile vile, alianza kampeni kali katika mtandao wa Twitter, akishinikiza kukabiliwa kwa mwanahabari huyo kisheria.
Kulingana na Bw Mochama, vitendo hivyo vilimharibia sifa na kumhatarishia kupoteza ufadhili wa masomo yake. Vile vile, alichunguzwa na polisi. Aliiambia mahakama kwamba, aliharibiwa jina, kwani alisawiriwa kama mbakaji.
Hata hivyo, Prof Mwangi alikanusha kuandika jumbe hizo katika mitandao ya kijamii. Badala yake, alisema jumbe alizoandika ni za kweli, kwani alizingatia uhuru wa kujieleza kama ilivyo katika Katiba.
Na licha ya Bw Mochama kukanusha kuwa alimdhulumu kimapenzi Bi Patel, Prof Mwangi alisisitiza kuwa mwanahabari huyo alifanya kitendo hicho mara kadhaa alipozuru makazi ya rafikiye.
Bw Mochama alidaiwa kufanya kitendo hicho kwenye Kikao Maalum cha Ushairi, Africa Poetry Book Fund kilichoandaliwa na mwasisi wake Prof Kwame Dawes.
Hata hivyo, hakimu alisema uhuru wa kujieleza haumpi mtu haki ya kutoa matamshi bila mipaka au kutathmini athari zake. Alisema kuwa lazima angetilia mkazo haki ya siri ya mtu.
“Nimetathmini kwa kina msingi wa kisheria baada ya kuangalia jumbe zilizoandikwa. Sina shaka yoyote kwamba jumbe hizi zilimrejelea Bw Mochama kwa kumtaja kama mbakaji. Hiyo ndiyo maana anayopata yeyote aliyesoma jumbe hizo,” akasema hakimu.
Na ingawa hakimu alieleza hakukuwa na ushahidi wowote kuonyesha mwanahabari huyo alimdhulumu kimapenzi mlalamishi, alisema kuwa wanawake hao wangepaswa kufahamu kuwa si haki kuandika jumbe za kumharibia mtu katika mitandao ya kijamii bila ushahidi wowote au msingi wa kisheria.
Alisema ikiwa wawili hao hawangekabiliwa vilivyo, kuna uwezekano wao kuendelea kuandika jumbe kama hizo bila majuto. Vile vile, aliwaagiza kuandika ujumbe wa kuomba msamaha kwa Bw Mochama kwa muda wa wiki mbili.