Mwanajeshi, polisi 3 ndani kuhusiana na wizi wa Sh72m
Na STELLA CHERONO
AFISA mmoja wa Jeshi la Kenya (KDF), na maafisa watatu wa polisi kutoka familia moja, wanazuiliwa kuhusiana na wizi wa Sh72 milioni kutoka benki ya Standard Chartered katika eneo la Nairobi West, Kaunti ya Nairobi.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema kuwa makachero walimkamata Bw Simon Gichuhi Karuku na mkewe, Bi Caroline Njeri, ambao wote ni maafisa wa polisi eneo la Thogoto, Kaunti ya Kiambu.
Makachero waliwakamata wawili hao katika afisi moja ya wakili, walikokuwa wameenda kumwagiza awasilishe ombi kortini kuzuia wasikamatwe.
Baada ya kukamatwa, washukiwa waliwapeleka makachero nyumbani kwa dada ya Bw Karuku, aliyetambuliwa kama Eunice Wangari Karuku. Bi Wangari ni mwanajeshi katika kambi ya kijeshi ya Kahawa jijini Nairobi. Bi Karuku ndiye alikabidhiwa pesa hizo.
“Afisa huyo alikuwa amesafiri mjini Nyahururu kuhudhuria mazishi,” walisema polisi.
Bi Wangari aliwaelekeza kwa dada yake, Bi Florence Wanjiru Karuku kuchukua fedha hizo. Bi Wanjiru pia ni afisa wa polisi ambaye alikuwa akilinda ATM ya Benki ya Equity, iliyo karibu na benki ya StanChart, wakati fedha hizo zilipoibwa.
Wakati polisi walipofika kwake, aliwaambia kuwa alipopata fedha hizo, alimpa mpenzi wake, aliyetambuliwa kama James Macharia, aliyetorokea sehemu isiyojulikana.
Makachero pia walipata gari aina ya Toyota Mark X, lenye nambari ya usajili KBX 779 kutoka kwa Bi Wangari, wanaloamini lilinululiwa kwa fedha hizo.
Wanne hao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata, huku polisi wakiendelea kumsaka Bw Macharia, anayeaminika kuwa na fedha zilizobaki.
Wizi huo ulifanyika mnamo Septemba 5, ambapo kulingana na taarifa za walinzi, “ulitekelezwa na watu waliovalia sare za polisi wa utawala.”
Fedha hizo ziliibwa baada ya wafanyakazi wa kampuni ya G4S kuziweka kwenye mashine ya ATM.
Walinzi wa G4S walikuwa wamesafirisha fedha hizo kutoka makao yao makuu yaliyo katika eneo la Industrial Area hadi Benki ya Standard Chartered tawi la Nairobi West.
Wezi wadhaniwa polisi
Taarifa kutoka kwa walinzi hao zilisema kuwa walidhani kuwa wezi hao walikuwa polisi waliokuwa wamesindikiza fedha hizo.
Wezi hao walipakia fedha hizo katika magunia 13, na kuyaweka kwenye gari ndogo walilokuwa nalo na kuondoka.
Siku chache baada ya wizi huo, polisi waliwakamata maafisa wawili wa polisi waliotambuliwa kama Chris Ayienda na Vincent Owuor, waliopatikana na Sh7 milioni. Vilevile walipata gari.
Makachero pia walipata Sh1 milioni katika zizi la ng’ombe katika eneo la Lurambi, Kaunti ya Kakamega.
Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya G4S aliyetambuliwa kama Bernard Sewanga, aliyekuwa ameenda mafichoni baada ya wizi huo pia alikamatwa.
Aidha, walipata Sh2.3 milioni katika nyumba ya Bi Mary Kyalo, mwenye umri wa miaka 60 katika Kaunti ya Machakos.
Mjukuu wake, Bernard Mwendwa pia alikamatwa.
Washukiwa wengine waliokamatwa kufikia sasa ni Musa Rajab, Abraham Mwangi Njoroge, Ascar Kemunto, Dancun Luvuka, Wilfred Nyambane, Natahn Njiru, Danmark Magembe, Boniface Mutua, Alexander Mutuku na Francis Muriuki.