Mwanamke ajifungua ndani ya teksi nje ya Nation Centre
FAITH NYAMAI na CHARLES WASONGA
MWANAMKE mmoja Jumanne jioni alijifungua mtoto mvulana ndani ya teksi nje ya afisi kuu ya Shirika la Habari la Nation Media Group (NMG) jumba la Nation Centre, jijini Nairobi.
Kulingana mfanyakazi wa NMG aliyeshuhudia tukio hilo, walijulishwa na dereva wa teksi ambaye alisimamisha gari hili na kuomba msaada.
Bi Evelyne Atieno ambaye ni mhudumu idara ya usafi katika jengo hilo ambaye alimsaidia mwanamke huyo alisema alikuwa akiondoka kuelekea nyumbani alipowasikia watu wakipiga kelele ndani ya gari nyeupe.
Mbeleni, alisema alidhani kuwa walikuwa ni wezi ambao walikuwa wakimpora mtu ndani ya gari hilo.
Kwa uangalifu, Bi Atieno alimua kuenda kuchungulia kupitia dirishani.
“Lakini nilipochungulia ndani ya gari hilo, niligundua kuwa mwanamke mmoja alikuwa akijifungua. Niliamua kumsaidia,” akasema.
Alisema aliamua kutumia leso yake na baada ya muda wanawake wengine wakaja na kuzingira gari hilo ili kulinda usiri wa mwanamke huyo.
Baada ya muda mfupi, daktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Meridian iliyoko katika orofa ya 11 waliwasili kutoa msaada wao.
Hii ni baada ya walinzi kuwapasha wataalamu hao kuwapasha habari wahudumu hao wa afya.
Wanawake wanaofanyakazi na mwanamke huyo walisema alianza kulalamikia maumivu tumboni majira ya jioni.
“Aliniamba, alihisi kama kwamba mtoto alikuwa anataka kutoka. Nilishtuka na ndipo tukaanza kusaka gari la kumkimbiza hospitalini,” akasema mama huyo.
Alisema aliitisha teksi ya Uber impeleke mwanamke huyo katika Hospitali ya Nairobi West, lakii kabla ya wao kufika karibu na jumba la Nationi Centre mama huyo alilemewa.
“Ilitubidi tusimamishe teksi na kuomba usaidizini,” akasema.
Mwenzake mama aliyefungua, alisema mume wa mama huyo alipigiwa simu na kujulishwa kuhusu tukio hilo.
Dereva wa teksi Bw Nelson Munene alisema alipigwa na butwaa mwanamke huyo alipoanza kujifungia ndani ya gari lake.
“Ilinibidi kusimamisha gari ili niruhusu wasamaria wema na wahudumu wa afya wamsaidie mama huyo,” akasema.
Akaongeza: “Hii ni mara yangu ya kwanza kushuhudia kisa kama hicho.”
Baada ya mama huyo kujifungua, yeye na mwanawe walipewa huduma ya kwanza katika hospitali ya Meridian.
Baadaye alipelekwa hadi katika hospitali ya Nairobi West kwa ambulansi, iliyoitwa na madaktari wa Meridian, kwa usaidizi zaidi.
Walioshuhudia kisa hicho waliwapongeza wahudumu hao wa afya na wahisani kwa kumsaidia mama huyo ambaye jina lake halikutambulika.