Habari Mseto

Mwanamke aliyelaghai watu mamilioni ya pesa na kutoroka miaka 10 asukumwa jela

Na RICHARD MUNGUTI March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UMATI mkubwa wa walalamishi wanaodai kuporwa mamilioni ya pesa kwenye kashfa ya mahindi ulikusanyika katika mahakama ya Milimani kushuhudia kushtakiwa kwa Teresia Wanjiru Boro aliyetoroka miaka 10 iliyopita.

Wanjiru aliyeshtakiwa kwa mara ya kwanza mahakama ya Thika 2015 kisha akatoroka, alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu Lucas Onyina mnamo Machi 24, 2025.

Bw Onyina alimnyima Wanjiru dhamana akisema mshtakiwa alitoroka huku walalamishi aliopokea pesa kutoka kwao wakidai aliwahadaa kwamba atanunua mahindi kupeleka kambi ya wakimbizi ya Kakuma.

“Hii mahakama inakataa ombi la dhamana ya Wanjiru ikitilia maanani kwamba alitoroka 2015 hadi wiki mbili zilizopita alipokamatwa tena kufuatia malalamishi mapya kwamba amepokea pesa kwa njia ya ulaghai kutoka kwa watu wengine akidai ni za kununua mahindi ya kupeleka kambi ya wakimbizi ya Kakuma,” Bw Onyina alisema.

Hakimu alikubaliana na kiongozi wa mashtaka Joyce Olajo kwamba mshtakiwa hastahili kuachiliwa kwa dhamana, kwa hofu ya kutoroka.

“Mshtakiwa alitoroka kwa mwongo mmoja (miaka 10) huku akiacha walalamishi vinywa wazi, bila pesa na mahindi,” Bi Olajo alimweleza hakimu.

Bw Olajo aliwasilisha ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia iliyosema kwamba mshtakiwa alitoroka mahakama ya Thika 2015, hadi wiki mbili zilizopita alipokamatwa kwa madai mapya ya ulaghai.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari-mseto/naibu-gavana-kiambu-ashtakiwa-kwa-kuzuia-mwili-wa-babake-uzikwe/

Hakimu alisema Wanjiru haaminiki tena na “njia ya kuhakikisha haki imetendeka ni kumzuilia mshtakiwa gerezani hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Bw Onyina alitupilia mbali tetesi za mshtakiwa kwamba “hakufika kortini kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19.”

Hakimu alisema, “Corona iliisha kitambo na mshtakiwa akaendelea kujificha na kukwepa haki.”

Aidha, aliamuru kesi ya Thika na kesi ya Milimani ziunganishwe Machi 28, 2025 zifanywe kama kesi moja.

Kwenye shtaka la kwanza, Wanjiru alikana kwamba alipokea Sh3.8 milioni kwa njia ya undanganyifu kutoka kwa Eva Waithira Kimuhu, akidai ni za kununua mahindi yaliyokauka kutoka maghala ya serikali ya Eldoret, Uasin Gishu.

Pia, alishtakiwa kwa kumlaghai Bernard Ngirita Chege Sh1, 145, 000 akidai ni za kununua mahindi.

Shtaka la tatu dhidi ya Wanjiru lilisema alipokea kwa njia ya undanganyifu Sh 581, 000 kutoka kwa Bw David Kamau Kimemia akidai ni za kununua mahindi yaliyokauka kutoka Eldoret.

Baada ya kuagizwa azuiliwe gereza la wanawake la Langata, walalamishi walipiga makofi huku wakisema “hatimaye tutapata haki.”

Mshtakiwa atarudishwa kortini tena Machi 28, 2025 kushtakiwa upya.