Habari Mseto

Mwanamke ampa mwanawe sumu kufuatia ugomvi na mume wake

Na SAMMY KIMATU April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

POLISI katika eneo la Makadara, Nairobi wanachunguza kisa cha uhalifu ambapo mwanamke katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina anadaiwa kugombana na mume wake na kwa hasira akampa mtoto wake wa miaka sita sumu kabla ya kunywa kiasi kikubwa cha sumu hiyo.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi wa Makadara, Judith Nyongesa, alieleza kuwa mtoto aliaga dunia na polisi wanaendelea na uchunguzi ili kukusanya ushahidi.

“Mtoto alifariki na mshukiwa mkuu alikimbizwa hospitalini ili kuokoa maisha yake. Hata hivyo, hakuweza kuzungumza lakini madaktari wanajitahidi kumhudumia. Tunamchukulia kama mshukiwa mkuu wa mauaji na tufungua mashtaka dhidi yake mara tu atakapopona,” Bi Nyongeza alisema.

Bi Nyongesa alisema kuwa mwili wa mtoto umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Nairobi Funeral Home ukisubiri kufanyiwa upasuaji.