Habari Mseto

Mwanamke atahiriwa lazima kama adhabu ya kuona uchi wa mwenzake

August 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA PETER MBURU

POLISI eneo la Igembe ya kati wanawasaka watu wanne ambao wanatuhumiwa kumtahiri mwanamke kama adhabu ya kuona uchi mwenzake ambaye amepashwa tohara.

Mwanamke huyo anadaiwa kutahiriwa kwa nguvu na mumewe pamoja na mavyaa na bavyaa wake, ambao baadaye walitoroka kuepuka kukamatwa.

Tukio hilo la Jumanne liliwaacha wakazi wa kijiji cha Mwiyo kwa mshtuko .

“Nilifahamu kuwa mawifi zake mdhulumiwa walikuwa wakipigana ndipo mmoja wao akavua nguo kutokana na hasira. Mdhulumiwa baadaye alikimbia kumsitiri wifi yake huyo huku akiwatuliza lakini baadaye bavyaa wake akaamrisha atahiriwe kwa ajili ya kuona uchi wa bintiye aliyepitia tohara,” akasema Bw Kithela Kubai, jirani.

 Bw Kubai alisema aliyetekeleza kitendo hicho anafahamika vizuri humo kijijini na kuwa amekuwa akihudumia kifungo cha nje baada ya kujaribu kumtahirisha mwanamke mwingine mwaka uliopita.

Naibu wa chifu wa kata ndogo ya Thuuru Bw David Mithea alisema juhudi za kuwatia washukiwa nguvuni ziliambulia patupu baada ya kuwakosa nyumbani kwao kwani tayari walikuwa wametoroka.

 “Tlifahamu kuhusu kisa hicho Alhamisi asubuhi lakini tulipofika katika boma hilo tulimpata mtoto tu. Huenda walitoroka baada ya kisa hicho kutangazwa katika kituo cha redio cha huku lakini bado tunachunguza kile haswa kilichochangia kitendo hicho,” akasema Bw Mithea.

Bw Kubai naye alisema alitumiwa vitisho na mumewe mdhulumiwa baada ya kuripoti kisa hicho.

Alisema kuwa visa vya utahirishaji wa wanawake vimekuwa vingi eneo hilo, akisema kimoja kiliripotiwa wiki iliyopita katika kijiji jirani cha Kithare.

“Haswa nyakati za likizo za shule visa hivi huwa vingi, mwaka uliopita tuliwaokoa wasichana sita kutoka vijiji vya Thuuru na Kathelwa baada yao kutahiriwa. Machifu eneo hili hawajaajibika,” akasema Bw Kubai.

Kisa hicho kilitokea siku chache baada ya mwenyekiti wa muungano wa Maendeleo ya Wanawake kaunti ya Meru Bi Mary Kanana kuwarai wakazi kukomesha visa hivyo.

Bi Kanana alisema uovu huo huendelezwa mara nyingi nyakati za likizo za Agosti na Disemba.

“Tunafahamu kuwa wazazi huwaficha wanao wa kike wakati wa kuwatahirisha lakini sasa tunamwonya yeyote atakayepatikana akiendeleza visa hivyo kuwa atachukuliwa hatua za kisheria,” Bi Kanana akasema.