Mwanamke azuiliwa akikabiliwa na shtaka la kumuua mumewe kwa sababu ya deni la Sh1,700
Na RICHARD MUNGUTI
MAMA wa watoto watano alifikishwa mahakamani kwa madai alimuua mumewe kwa sababu ya deni la Sh1,700.
Susan Kawira alimsihi hakimu mkuu Martha Mutuku aamuru akubaliwe kwenda gerezani na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano na miezi sita “kwa vile hakuna mtu anayeweza kumtunza.”
Lakini Bi Mutuku aliamuru afisa wa idara ya kuwachunga watoto amchukue mtoto huyo na amtunze hadi pale kesi ya mauaji dhidi ya Kawira itasikizwa na kuamuliwa.
“Huwezi ukakubaliwa kwenda rumande na mtoto. Haki za mtoto huyu zinakandamizwa. Hajakosea. Ni afisa wa watoto atakayekubaliwa kumtunza,” aliagiza Bi Mutuku.
Mahakama iliamuru Kawira azuiliwe kwa siku 14 kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi kuhusu mauaji ya mumewe Jackson Mwikya aliyekuwa na umri wa miaka 41.
Afisa wa polisi anayechunguza kesi hiyo Mathew Rono aliambia mahakama mauaji hayo yalifanyika katika mtaa wa Laini Saba, Kibra katika Kaunti ya Nairobi.
Mshukiwa huyo atazuiliwa hadi Juni 2, 2020.