Mwanamume afariki akiandaa mazishi ya mama yake
JACKSON Otieno Okuthe alikuwa akijiandaa kwa mazishi ya mama yake, Mary Auma, nyumbani kwao Kanyangasi, Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay.
Alikuwa amewasili kutoka Mombasa, ambako anafanya kazi kama ajenti wa kupokea na kusafirisha mizigo.
Alipofika, alishiriki mipango ya mazishi na kuhakikisha ndugu zake watavaa mavazi mazuri katika hafla hiyo. Pia, alikuwa amepeleka nguo kufuliwa mjini Homa Bay, akipanga kuzichukua kabla ya mazishi Aprili 4.
Mnamo Jumanne Machi 27 jioni, alipokuwa akitembea katika kituo cha mabasi cha Homa Bay ili kukutana na rafiki, aligongwa na matatu.
Alifariki alipofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.
Mwili wake sasa umelazwa katika mochari ya Med 25, pamoja na mwili wa mama yake, aliyefariki Machi 3.
Siku ya ajali, Jackson alikuwa ameenda Homa Bay Town kutengeneza gari lake lililokuwa na hitilafu.
Baada ya kuliacha gereji, alichukua bodaboda hadi duka la kufulia nguo na kisha akaelekea kwenye kibanda cha chakula karibu na kituo cha mabasi kula omena, chakula chake anachopenda.
Akiwa pale, alipokea simu kutoka kwa rafiki yake aliyekuwa upande mwingine wa kituo cha mabasi.
Alipojaribu kuvuka kwenda kumuona, aligongwa na gari lililokuwa likiendeshwa na kondakta wa matatu.
Walioshuhudia walisema waliskia kishindo kikubwa na walipofika, walimkuta Jackson akiwa chini ya gari. Walilazimika kuinua gari kwa mikono ili kumtoa kabla ya kumkimbiza hospitalini, ambako alithibitishwa kufariki.
Familia yake sasa inaomboleza vifo viwili kwa wakati mmoja.
Ndugu yake, Daniel Okuthe, alisema mama yao na kaka yake watazikwa pamoja Aprili 4.
Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Homa Bay, Emmanuel Kipalgat, alisema dereva wa gari lililosababisha maafa alikamatwa lakini aliachiliwa kwa dhamana na atafikishwa mahakamani mnamo Aprili 8.
Kondakta aliyetoroka bado anasakwa.
Familia na marafiki wanamlilia Jackson, wakimkumbuka kama mtu wa watu na mwenye moyo wa upendo.