• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Mwanamume afariki, wawili waponea baada ya moto ndani ya lojing’i

Mwanamume afariki, wawili waponea baada ya moto ndani ya lojing’i

MWANAMUME mmoja alifariki huku wengine wawili wakinusurika kifo kwa tundu la sindano baada ya moto kutokea ndani ya lojing’i walimokuwa.

Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi za usiku katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kamongo ulioko katika wadi ya Landi Mawe, Kaunti ya Nairobi.

Mwanamume huyo alikuwa akifanya kazi ya kurembesha kucha za wanawake katika Eneo la Viwandani na mitaani.

Kwa mujibu wa mmiliki wa vyumba hivyo vya kukodisha, Bi Hellen Wanza, 49, wakazi waliamshwa na nduru watu wakiomba msaada baada ya moto kutokea mwendo wa saa kumi za usiku.

“Inaaminika marehemu alisahahu kuzima mshumaa aliowakisha kabla ya kulala kwa vile hatuna stima ndani ya vyumba vyetu. Tulijaribu kuuzima moto lakini alikuwa ameuliwa na moshi kabla ya moto kuzimwa,” Bi Wanza akaambia Taifa Leo.

Tulifanya juhudi za kupata jina la marehemu lakini juhudi zetu hazikufua dafu kwani baada ya kwenda kwa mpangaji mwingine inakoaminika marehemu alikuwa akikodisha chumba, ni nguo chache zilizokuwa ndani ya mfuko uliokuwa hapo.

Hata hivyo, mmiliki wa vyumba hivyo, kwenye orofa za mabati, Bi Catherine Kawira, 38 alisema marehemu alikuwa akilala kwa chumba chake kila siku lakini aliamua “kukwepa kwa sababu ana deni lake”.

“Leo hakuja kwangu kwa sababu ninamdai ndiposa aliamua kukodi chumba mahali kwingine,” Bi Kawira akasema.

Vyumba hivyo hukodishwa kwa Sh50 usiku mmoja na wateja wake hasa huwa ni makanga na wengine wafanyao kazi za sulubu na juakali mitaani.

Ni katika eneo la mkasa pia ambapo mwanamume aliuliwa kufuatia mzozo ndani ya baa alipogongwa kwa kiti na kujeruhiwa kichwani miaka mitatu iliyopita.

Polisi wameanzisha msako wa kubaini ukweli wa mambo huku mwili wa marehemu ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City, Kaunti ya Nairobi.

You can share this post!

Mchuano kati ya Nairobi Stima na Posta Rangers kuamua timu...

Jericho All Stars yazidi kuwika

adminleo