Habari Mseto

Mwanamume apokonywa mke na pasta aliyesimamia harusi yake

August 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KNA

MFANYABIASHARA mmoja kutoka eneo la Juja Farm, Kaunti ya Kiambu, anasononeka baada ya mkewe wa miaka 26 waliyejaliwa watoto watano kunyakuliwa na pasta aliyesimamia harusi yao.

Bw John Kanyua ameshindwa kuelewa ni vipi pasta aliyewasaidia wakati wa ndoa yao, hata akatia saini cheti chao cha harusi, alimnyelea mkewe wa zaidi ya miongo miwili.

Mwanamume huyo hakutambua kuwa pasta huyo alikuwa akimezea mate mkewe, Leah Wambui, kwa miaka hiyo yote licha ya baadhi ya waliohudhuria harusi yao kubaini ukweli huo.

Hayo yote yalianza wanandoa hao walipoanza kuhudhuria kanisa la pasta huyo eneo la Juja Farm.

Na baada ya kupendezwa na mchango wao kanisani, pasta huyo alimteua Leah kuwa naibu wake katika Kanisa hilo, jambo lililofanya mke wa pasta kuingiwa na wasiwasi.

“Nilipinga uteuzi, lakini alinipuuzilia mbali. Nilimkabili Leah na kumwonya dhidi ya kucheza na mume wangu. Alionekana asiye na hatia, na nikakubali,” alisema Agnes Wangivi, mke wa pasta huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye wamejaliwa watoto watatu.

Urafiki kati ya Leah na pasta uliendelea kunawiri kiasi kwamba, kiongozi huyo wa kanisa angemwalika (Leah) nyumbani kwao kwa hafla za kifamilia, lakini bila kuandamana na mumewe.

“Hapa ndipo nilianza kuuliza maswali kuhusu urafiki wao. Nilimkabili Kinyua na kumwambia amwambie mkewe aachane na mume wangu, lakini hakuwa makini. Hatimaye mume wangu alitelekeza familia yake na kutoweka na Leah mnamo 2015,” Bi Wangivi aliongeza.

Kanyua anasema kuwa hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba, mara kadha pasta huyo angefika nyumbani kwake asubuhi na kusalia mle mchana kutwa na mkewe wakiwa wamejifungia chumbani.

Hii ilimfanya kuwaita maafisa wa utawala na viongozi wa kanisa ili wamsaidia kutatua shida hiyo.

“Hali ilikuwa mbaya kwani pasta alitoroka na mke wangu pamoja na watoto na wakakodisha nyumba katika soko la karibu ambako wanaishi,” alisema.

Wataka kurejesha mahari

Wazazi wa Leah sasa wamewasiliana na Kanyua wakimtaka akubali warejeshe mahari aliyotoa kwao ili kutoa nafasi kwa harusi mpya ya binti yao, lakini mwamume huyo amekataa.

Pasta huyo pia amewaambia watoto wake kwamba, anapanga kuoa mke mwingine na kwamba ametengana na mama yao.

Licha ya kukabiliwa na shida hii, Kanyua bado hulipa karo ya watoto wake kando na kutuma chakula wanakoishi na pasta.

“Hii haiwezekani na siwezi kukaa nikitizama mtu mwingine akichukua familia yangu. Ikiwa serikali haitaingilia kati, nitaamua la kufanya. Nimegharimika pakubwa kutunza familia yangu kwa miaka hiyo yote. Sitaruhusu harusi hiyo kuendelea na nitawasilisha kesi ya kuipinga. Akome kuharibu jina lake na aombe msamaha, na nitamkubali arejee nyumbani,” alisema Bw Kanyua.