Habari MsetoSiasa

Mwanamume mbioni kuhakikisha muafaka wa Uhuru na Raila umegeuzwa sikukuu

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MWANAMUME mmoja ameshangaza kuandikia Bunge la Kitaifa barua akitaka siku ambayo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga waliweka muafaka wa maelewano mnamo Machi 9 ifanywe sikukuu ya kitaifa ya kusherehekea amani.

Bw Paul Mugo analitaka bunge kupitia kamati zinazofaa kubadilisha sehemu ya 9(3) ya katiba kuongeza tarehe hiyo kama sikukuu ya taifa, iwe ikisherehekewa kila Machi 9.

Bw Mugo anahoji kuwa kwa miaka mingi amani haijakuwa kitu cha kupatikana kwa urahisi humu nchini, na hivyo salamu iliyoleta muafaka baina ya viongozi hao wawili imekuwa chanzo cha utangamano, kuishi kwa amani baina ya jamii na utaifa.

“Cha muhimu zaidi ni juhudi za serikali na upinzani ili kuafikia malengo makuu manne na kuafikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini,” barua ya Bw Mugo ikasema.

Barua hiyo imetumwa kwa kamati ya bunge kuhusu haki na masuala ya sheria ambayo itaipitia na kutoa ripoti bungeni kati ya kipindi cha siku 60.

Katika muafaka wao wa awali mwaka huu, viongozi hao walielewana kuzika tofauti ambazo zimekuwa zikiwatawanya Wakenya, haswa kila baada ya Uchaguzi Mkuu, ili kuimarisha ugatuzi, kuwahusisha watu wote katika uongozi wan chi na kushughulikia suala la uhasama wa kikabila.