Habari Mseto

Mwanariadha kortini kwa madai ya kujaribu kufyeka mkewe kwa panga

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JOSEPH NDUNDA NA PHILIP MUYANGA

MWANAUME aliyedaiwa kujaribu kumshambulia mkewe kwa panga wakati wa mzozo wa kinyumbani, Kaunti Ndogo ya Njiru, Nairobi, atasalia rumande hadi Februari 14, baada ya kukana mashtaka hayo.

Mshtakiwa Stanley Kipkemoi alikuwa amefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu, Bw Tito Gesora wa Mahakama ya Makadara.

Alishtakiwa kwa kujaribu kumuumiza Luiza Lenantoiye, na jaribio la kutaka kukata mwanawe kichwa, Januari 26 baada ya kurejea usiku.

Bw Kipkemoi alikuwa ameondoka nyumbani baada ya mkewe kumwamrisha atafute kazi badala ya kukaa ndee nyumbani.

Wakati huo huo, kesi ambapo Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) kimeshtakiwa kwa madai ya kuchapisha picha za wahitimu watatu wa Chuo Kikuu cha Moi nyuma ya kijitabu chao cha kuhitimu bila kibali, itashughulikiwa kwa njia ya upatanisho.

Hii ni baada ya Jaji Olga Sewe kuuliza pande zote ikiwa zinakubali kuendeleza upatanisho.

Kupitia kwa mawakili Hamisi Mwadzogo na Abdulkadir El-Kindy wa TUM na wahitimu hao watatu mtawalia, pande zote ziliambia mahakama kuwa zinaweza kuendeleza upatanisho.

Jaji Sewe aliagiza hati za kesi hiyo kutajwa mbele ya Naibu Msajili wa mahakama.

Bi Nawal Ali, Bw Abad Hanzuwan na Bi Fatima Athman waliishtaki TUM kwa madai ya kuchapisha picha hizo bila ya wao kujua, kuwaomba ridhaa au mamlaka, kinyume na sheria.

Hapo awali, chuo kikuu kiliomba suala hilo litatuliwe nje ya mahakama.

Katika ombi lao katika Mahakama Kuu ya Mombasa, Bi Nawal, Bw Hanzuwan na Bi Athman wanaomba agizo kwamba TUM ilazimishwe kuwalipa fidia kwa uharibifu au hasara inayotokana na uchapishaji wa picha zao bila idhini yao.