Mwanaume auawa Bomet kwa kukataa kulipa yai la Sh25
MWANAMUME ameuawa na mchuuzi wa mayai katika baa moja iliyoko kijiji cha Mogogosiek, Bomet baada ya kudinda kulipa yai la Sh25.
Brian Moi, 20 aliagiza yai moja kutoka kwa mchuuzi huyo ili apunguze ulevi. Lakini baada ya kulila yai hilo alikataa kumlipa mchuuzi huyo na hapo ndipo wawili hao wakaanza kubishana.
Walioshuhudia kisa hicho walisema wawili hao walibishana vikali hadi Moi akagonga toroli ya mchuuzi huyo na kumwaga Kachumbari anayotumia kuongezea mayai ladha
“Mchuuzi huyo alipandwa na hasira baada ya Moi kumwaga Kachumbari. Ghafla bin vu alichomoa kisu na kumdunga kwenye kifua,” mmoja wa mashahidi hao, Bw Kipkoriri, akaeleza.
Mchuuzi huyo alitoroka baada ya kutekeleza kitendo hicho. Moi, ambaye alikuwa akivuja damu kwa wingi, alikimbizwa katika Hospitali ya Litein kwa matibabu lakini alikata roho dakika chache baadaye.
Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Bomet, Edward Imbwaga alithibitisha kuwa Moi aliuawa kwa kudungwa kisu kuhusiana na Sh25 alizodaiwa baada ya kula yai la mchuuzi mmoja.
“Tumemkamata mchuuzi huyo wa mayai na ‘smokies’. Anazuiliwa korokoroni na atafikishwa mahakamani,” akasema Bw Imbwaga.
Mamake Moi Florence Ngetich alisema familia yake imehuzunishwa na tukio hilo na wanasaka haki kwa mauaji ya mpendwa wao.
“Nimejawa na huzuni kuu. Mtoto wangu hakuwa mgonjwa, aliuawa kinyama na nitataka haki itendeke,” akasema huku machozi yakimdondoka.
Babake Moi, Geoffrey Ngetich alielezea kushangazwa na tukio hilo aliuliza ni vipi mabishano kuhusu jambo dogo yalisababisha kifo.
“Brian alitaka yai moja tu. Lakini kwa sababu nyakati nyingine vijana huingiwa na makeke, akamwaga Kachumbari. Hapo ndipo mchuuzi huyo alimdunga kwa kisu. Kama familia tunataka jamii huyo aadhibiwe kwa mujibu wa sheria,” akasema Bw Ngetich.
Kisa hicho kilivutia hisia za viongozi wa eneo hilo wakiwemo Seneti Hillary Sigei na Mbunge wa Konoin Brighton Yegon waliotembelea familia kuwapa pole.
“Tunasimama na familia hii katika kushinikiza kwamba haki itendekeza kufuatia mauaji ya kinyama ya kijana Brian Moi,” akasema Bw Sigei.
“Sharti tushirikiane kama jamii kuhakikisha kuwa maafa hayatokei tena katika hali kama hii,” Seneta huyo akaongeza
Kamishina wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) Isaac Ruto pia alilaani kisa hicho akieleza kuwa huwa na shughuli mara kadhaa katika eneo hilo.
“Hili ni tukio la kusikitisha zaidi. Natuma rambirambi zangu kwa familia ya mwendazake. Matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya yamekithiri zaidi katika kaunti ya Bomet. Ninatoa wito kwa vijana kudumisha amani kuzuia matukio kama haya,” akaeleza Bw Ruto.