Habari Mseto

Mwandishi wa Pakistan achapisha kitabu kuhusu Mkenya mpenda wanyama

April 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

 Na MAGDALENE WANJA

Mwandishi wa vitabu vya watoto kutoka nchi ya Pakistan Bi Nusser Satyeed amechapisha kitabu kinachosimulia hadithi ya Mkenya Patrick Kilonzo ambaye ametambulika kwa juhudi zake za kulinda maisha ya wanyamapori.

Katika kitabu hicho chenye jina The Waterhole, hadithi ya Bw Kilonzo inatumika kama kielelezo cha kuwaelimisha watoto kuhusu umuhimu wa kuwahifadhi wanyama pori.

Kitabu hicho kimetumia michoro ya wanyama mbali mbaliambao walifaidika kutokana na ukarimuwa Bw Kilonzo.

Bw Kilonzo anayefahamika kama “Waterman of Tsavo” alipata jina hilo kutokana na kitendo chake cha kuwapa wanyamapori maji katika mbuga ya Tsavo wakati wa kiangazi.

 Alichota maji kwa kutumia gari la maji wakati chemichemi za maji zilikauka kana kuwaacha wanyama wengi kuangaika katika mwaka wa 2016.

“Nilikuwa nikichota maji kutoka ka umbali wa kilomita 70 na kuileta ndani ya mbuga ambapo wanyama wa aina mbalimbali waliweza kujifaidi nayo,” alisema Bw Kilonzo.

Bw Kilonzo amefanya kazi ya kujitolea kuwahifadhi wanyama pori katika mbuga kwa zaidi ya miaka 14.

“Niligundua kuwa wanyama walikosa namna ya kukata kiu na wengine walipoteza maisha yao kuokana na ukame huo, na kinyume na binadamu amabao wana uwezo wa kuitisha msaada, wanama hawakuwa na namna nyingine,” alisema Bw Kilonzo.

Mwaka mmoja uliopita, Bw Kilonzo pia alianzisha mradi mwingine wa kupunguza mgogoro kati ya wanyama na binadamu wanaoishi karibu na mbuga kwa kupanda alizeti.

Bw Kilonzo alisema kuwa mradi huo amabao unategemea maji ya mvua tayari umeanza kuzaa matunda kwani wanyama pori hawawasumbui tena wakazi wa eneo hilo.

“Hapo hawali, wanyama walikuwa wakivamia mashamba na kuwaacha wakulima na hasara kubwa lakini hayo yamebadilika kwani wanyama hao haswa ndovu hawali alizeti,”alisema Bw Kilonzo.

Aliongeza kuwa kando na kupunguza mgogoro, wakulima pia wanapata faida baada ya kuuza alizeti ambazo wanauzia kampuni za kutengeneza mafuta.