Mwaniaji urais aliyejaribu kujiua kujua hatima yake Agosti
Na RICHARD MUNGUTI
MWANIAJI kiti cha urais mwaka wa 2017 wa kujitegemea Bw Peter Solomon Gichira atajua hatima ya kesi inayomkabili ya kujaribu kujiua mnamo Agosti 30, 2019.
Hakimu mkuu wa mahakama ya Nairobi Francis Andayi aliyesikiza kesi hiyo alimweleza Bw Gichira kuwa hajakamilisha kuandaa uamuzi wa hiyo inayomkabili ya kujaribu kujitoa uhai mnamo Mei 27 2017..
Bw Gichira anayetetewa na wakili wa Nairobi alimweleza hakimu “hapingi uamuzi ukisongezwa hadi Agosti 30, 2019.”
Mwaniaji huyo wa kiti cha urais alijaribu kujirusha kutoka orofa ya sita katika jengo la Anniversary, Nairobi baada ya kutokubaliwa kushiriki katika kinyang’iro cha urais.
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Wafula Chebukati alikataa kupokea makaratasi yake kwa vile hakuwa na wapendekezaji milioni mbili kama inavyotakiwa kisheria.
Pia Gichira alifika katika kituo cha uteuzi cha KICC kama amechelewa.
Mwaniaji huyo alitamauka na kujawa na hasira za mkizi ndipo akatisha kujitoa uhai na pia kusababisha uharibifu wa mali na kuhatarisha amani.
Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana ya Sh200,000. Aliposhikwa alikaa siku mbili katika kituo cha polisi cha Central kabla ya kufikishwa mahakama ya Milimani.
Alishtakiwa kuharibu mali ya IEBC yenye thamani ya Sh30,000.
Pia alidaiwa alihatarisha amani kwa kufika katika afisi za IEBC kudai sababu ya kuitishwa saini za wawaniaji huru zaidi ya 48,000.