Habari Mseto

Mwathethe awataka waliofuzu KMA kujizatiti kuifaa nchi

April 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MAOSI NA FRANCIS MUREITHI

MKUU wa Majeshi nchini Jenerali Samson Mwathethe, Alhamisi aliongoza hafla ya kufuzu kwa maafisa wa kijeshi katika kambi ya Lanet, Kaunti ya Nakuru.

Sherehe yenyewe ilifanyika katika chuo cha mafunzo ya kijeshi, Kenya Military Academy (KMA).

Zoezi la kuwanoa makurutu huchukua miezi sita kabla ya wao kuhitimu, kisha huaanza kuhudumu katika nyanja mbalimbali jeshini.

Waliohitimu huwa wamejipatia ujuzi wa kufanya kazi kama vile utabibu, uanahabari, uhandisi au viongozi wa kidini.

Baadhi ya makurutu wa kijeshi waliohitimu kwenye hafla iliyofanyika Kenya Military Academy, Lanet. Picha/ Richard Maosi

Usalama wa hali ya juu ulikuwa umeimarishwa huku familia za wale tu waliofuzu na wanahabari wakiruhusiwa kuhudhuria.

Bali na wanafunzi kufuzu, baadhi yao walitambuliwa kutokana na mchango wao mkubwa nje ya mafunzo ya kijeshi.

Abunidal Ahmed Mohammed aliibuka kuwa mwanafunzi bora katika kozi ya masomo ya kitaaluma huku Catherine Akinyi akichukua nambari mbili katika tuzo hizo maalum zinazotolewa kwa hisani ya serikali ya kitaifa, kwa ushirikiano na kambi za kijeshi.

Jenerali Mwathethe aliwataka wanafunzi kutumia ujuzi wao kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

 

Bendi ya kijeshi ikiwatumbuiza wageni waliofika kushuhudia wanao wakifuzu. Picha/ Richard Maosi

Aliwaomba kushirikiana na serikali ili wasaidie kupambana na magenge ya kigaidi yanayotishia nchi hususan mipakani.

Pia alieleza kuwa serikali imejitolea kupigana na wahalifu kutoka Somalia, ambao kwa siku nyingi wamekuwa wakitishia uwekezaji humu nchini.

“Ni wajibu wetu kama wataalamu katika kitengo cha usalama kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha mipaka yetu inalindwa dhidi ya magaidi na kuwakabili,” alisema.

Alieleza kuwa taasisi ya kijeshi ilikuwa na zana ,pamoja na maafisa wa kutosha kupambana na maadui. Aliwataka makurutu kuwa wazalendo na kujivunia nchi yao licha ya misukosuko mingi.

Wazazi wafika kuwapongeza wanao waliofuzu. Picha/ Richard Maosi

Kabla ya sherehe kukatika, bendi ya kijeshi ilichukua muda kuwatumbuiza wageni waliofika kushuhudia wapendwa wao wakijiunga na idara ya utumishi kwa taifa.

Ilifuatwa na makurutu kula kiapo mbele ya Jenerali Mwathethe aliyefika kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyatta.

KMA ilibuniwa mnamo 1941 na kubatizwa jina la Sajini Leakey Barracks aliyeuawa katika nchi ya Uhabeshi akiwa kazini.

Baada ya Uhuru idara ya kutoa mafunzo maalum, ilihamishwa hadi Lanet viungani mwa mji wa Nakuru.

Idara hii iliendelea ilipanua wigo na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaotokea ukanda wa Afrika Mashariki.

Catherine Akinyi (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Jenerali Samson Mwathethe. Picha/ Richard Maosi

Kufikia 1970 ilibadilishwa jina na kuitwa Armed Forces Training College(AFTC) AFTC ilipatiwa jukumu la kufundisha maafisa wanaosimamia shughuli kwenye kambi pamoja na wanafunzi waliozamia kwenye taaluma kando na zile za kijeshi.

Ilipofika 1998 KMA walianza kuchukua wanafunzi kutoka mataifa jirani ya Botswana, Burundi, Malawi, Swaziland, Rwanda Tanzania na Uganda.

Kozi ya kufundisha maafisa pekee ilihamishwa hadi Kahawa Karen mjini Nairobi.

Tangu kambi hii ianzishe mafunzo ya shahada,walibadilisha nembo yao kutoka AFTC na kuipatia rasmi jina la Kenya Military Academy.

Maafisa wa kijeshi wakionyesha ujuzi wao mbele ya umati. Picha/ Richard Maosi

KMA hutoa mafunzo ya kijeshi mbali na kuwakuza wanafunzi katika uwanja wa utumishi kwa taifa,lakini wengi wao huishia kufanya kazi jeshini.

Hali hii imesaidia kambi za kijeshi kuziba pengo kati ya raia wa kawaida na maafisa wa kijeshi na kupoteza dhana kuwa hawawezi kufikika.

Maafisa wake wengi wako nchini Somalia kukabiliana na kundi la Al-Shabaab tangu utawala wa serikali ya muungano ya Mwai Kibaki na Raila Odinga.