Mwili wa msichana wapatikana kwenye shimo la maji-taka Lamu
Na KALUME KAZUNGU
MWILI wa msichana aliyekuwa na umri wa miaka mitatu ambaye aliripotiwa kutoweka kwa siku tatu Lamu hatimaye umepatikana kwenye shimo la maji-taka.
Aziza Muhammad Alwy, mkazi wa mtaa wa Riyadha mjini Lamu, alitoweka muda mfupi baada ya kufika eneo la Bombay akiwa ameandamana na mamake wakati wakizuru mmoja wa jamaa zake eneo hilo alasiri ya Februari 19, 2020.
Juhudi za wazazi wake pamoja na watu wa nasaba yake kumtafuta ziligonga mwamba, hatua ambayo iliwasukuma wazazi wa msichana huyo kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi cha mjini Lamu kupitia nambari ya OB 06/20/2/2020.
Akithibitisha kupatikana kwa maiti ya msichana huyo, Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Moses Murithi, alisema walipokea ripoti kutoka kwa wananchi kwamba kulikuwa na mwili wa mtoto mdogo uliokuwa ukielea kwenye shimo la maji-taka eneo hilo la Bombay.
“Ilikuwa yapata saa nne asubuhi tulipopokea ripoti kutoka kwa wananchi kwamba walikuwa wameupata mwili wa msichana wa miaka mitatu aliyekuwa awali ameripotiwa kutoweka,” akasema Bw Murithi.
Alifafanua kwamba mwili ulikuwa ukielea kwenye shimo la maji-taka mtaani Bombay.
“Maafisa wetu walifika pale na kuthibitisha; na wakisaidiana na wananchi, walifaulu kuutoa mwili huo na kuusafirisha kwenye hospitali ya rufaa ya King Fahad ili ufanyiwa upasuaji wa maiti,” akasema akiongeza tayari wameukabidhi mwili kwa familia ili kuuzika kulingana na utaratibu wa dini ya Kiislamu.
Aliongeza kwamba uchunguzi unaendelea.
Baadhi ya wakazi waliohojiwa na ‘Taifa Leo’ aidha walishuku huenda msichana huyo aliuawa mahali kwingine kabla ya mwili wake kutumbukizwa kwenye shimo hilo la maji-taka.
“Kulingana na uzoefu wetu, miili inayoelea baada ya watu kufa maji huwa inaelea kwa upande wa mgongo na wala si kingalingali kama tulivyoshuhudia maiti ya msichana huyu. Hiyo ni dhihirisho tosha kwamba msichana hakufa maji. Kuna uwezekano aliuawa mahali kwingine na maiti yake ikatupwa kwenye shimo hili la maji-taka,” akasema Bw Mohamed Omar.
Wakazi aidha wameitaka idara ya usalama, Kaunti ya Lamu kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo msichana huyo aliuawa na kuhakikisha kuwa waliotekeleza unyama huo wanatiwa mbaroni na kuadhibiwa.
Wakati huo huo, wakazi wameiomba serikali ya Kaunti ya Lamu kufunika au kuzingira ua mashimo na visima vyote vilivyoachwa wazi kwenye mitaa mingi ya kisiwa cha Lamu.
Bi Umi Abdalla alisema kuwepo kwa visima na mashimo hayo kunahatarisha maisha ya watoto wadogo na watu wazima ambao mara nyingi huishia kutumbukia ndani.
“Tunaiomba serikali ya kaunti kufikiria kuzingira ua au kuvijengea ukuta visima na mashinmo yote yaliyoko Lamu. Yamekuwa kero hasa kwa watoto na wazee ambao mara nyingi hutumbukia ndani na kufariki,” akasema Bi Abdallah.
Maeneo ambayo visima na mashimo mengi yako wazi na kuhatarisha maisha ya wakazi ni pamoja na Kashmir, Bombay, Kandahar, Gadeni, Langoni na sehemu zingine za kisiwa cha Lamu.