Habari Mseto

Mwongozo wa kununua bidhaa NYS ulikuwa na dosari, korti yaambiwa

January 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa masuala ya usimamizi katika Wizara ya Ardhi Bw Julius Kiplagat Kandie Jumatano alikiri kwamba mwongozo uliopewa wakuu wa wizara na mashirika ya Serikali ulikuwa na kasoro.

Akitoa ushahidi katika kesi ya kashfa ya Sh60 milioni dhidi ya katibu wa zamani Lillian Omollo, Bw Kandie alimweleza hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko kuwa hakuna njia watekelezaji wa mwongozo huo wangeukwepa.

Bw Kandie aliwaondolea lawama Bi Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS Bw Richard Ndubai na washkiwa wengine 31 wanaoshtakiwa kwa ufujaji wa Sh60 milioni akisema , “hakuna namna wangeukosoa mwongozo huo.”

Alisema akiwa mwenyekiti wa kamati iliyoteuliwa kubuni mwongozo wa ufunguzi wa zabuni, masharti na sheria za utenda kazi (MTC) aliandaa taarifa iliyopelekewa wizara na mashirika ya Serikali.

“Ilibidi tu makatibu na wakuu wa mashirika ya serikali kutii na kuutekeleza mwongozo huo jinsi ulivyo hata ikiwa ulikuwa na dosari,” alisema Bw Kandie.

Akijibu maswali kutoka kwa wakili Migos Ogamba, Bw Kandie alisema wakuu serikalini na wakurugenzi wa mashirika ya Serikali hawakuwa na budi ila kutekeleza taarifa hiyo pasi kuihoji.

“Kukaidi mwongozo huu ilikuwa sawa na kuhoji na kukosoa mamlaka makuu ya nchi,” Bw Ogamba alimwuliza.

Bw Kandie alisema wanachama wa MTC walikuwa wanateuliwa na Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi.

Bw Kandie alisema mwongozo huo ulibuniwa 2012 na waliouteuliwa 2016 waliutumia ukiwa na dosari hizo.

Akitoa ushahidi katika kesi ya kashfa ya NYS ya Sh60milioni, Bw Kandie alisema dosari katika mwongozo ulikuwa tu unarithiwa na wizara zote na wakuu wa mashirika.

Alisema dosari hiyo ilipelekea serikali kupoteza mamilioni ya pesa.

Mawakili walimweleza shahidi huyo makosa aliyofanya na kamati ya MTC ndiyo yalipelekea umma kupoteza viwango vikubwa vya pesa na kwamba ni yeye angelifaa kuwa kizimbani.

Bi Omollo, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Bw Richard Ndubai  na washukiwa wengine  25 wameshtakiwa kwa kosa la kufanya njama za kuibia NYS Sh60,598,800 kati ya Aprili 6 2016 na Aprili 27 2017.

Bi Omollo ameshtakiwa kwa kosa la kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya kwa kuwalipa kimakosa Bi Catherine Njeri kamuyu, Sarah Murungu Andrine na Grace Nyambura Mbare wamiliki wa kampuni ya Erastz Enterprises Sh26,600,000.

Anakabiliwa na shtaka lingine la kuruhusu kampuni ya Arkroad Lrd kulipwa Sh24,866,800.

Bi Omollo na washukiwa hao wengine wamekanusha mashtaka ya utumiaji wa mamlaka yao vibaya. Wako nje kwa dhamana.

Kesi inaendelea kusikizwa.