Mzozo wa wanamuziki kutoka Mlima Kenya wafanya kikao chao na Uhuru kufutwa
NDUNGU GACHANE na VALENTINE OBARA
SERIKALI Jumapili ilifutilia mbali mkutano uliotarajiwa kufanyika kesho kati ya Rais Uhuru Kenyatta na wanamuziki wa eneo la Kati mwa nchi.
Msemaji wa serikali, Bw Eric Kiraithe, Jumapili alisema mkutano wowote utakaoandaliwa utahusu masuala yanayokumba sekta ya muziki kitaifa.
Tangazo hilo lilitolewa huku wanamuziki katika eneo la Kati wakizozana kuhusu mwaliko huo uliotolewa kwao na Rais Kenyatta wiki iliyopita wakati wa mazishi ya mwanamuziki Joseph Kamaru.
“Kufikia sasa serikali imepokea jumbe kutoka kwa zaidi ya wanamuziki 10,000 ambao wanataka kuhudhuria mkutano huo. Ajenda ya mkutano huo inafaa kujumuisha changamoto zote zinazokumba sekta ya muziki katika ngazi ya kitaifa,” akasema kwenye taarifa.
Aliongeza kuwa Wizara ya Michezo na Turathi imetakiwa kuunda jopokazi litakalopanga mkutano huo kwa njia ambayo wanamuziki wa nchi nzima watawakilishwa.
Mgawanyiko wa wanamuziki wa eneo la Kati ulikuwa kwamba upande mmoja ulikuwa unalaumu wenzao kwa madai kuwa wanataka kutumia mkutano huo kufanikisha masilahi yao ya kibinafsi.
Rais alipotoa mwaliko huo wiki iliyopita alikuwa anajibu ombi la Mbunge Maalumu, Maina Kamanda, ambaye alisema alitumwa na wasanii kumwomba kiongozi wa taifa akutane nao kujadili jinsi anavyoweza kuboresha hali yao ya kimaisha.
Mwanamuziki mashuhuri katika eneo la kati, Kamande Wa Kioi, alisema hafahamu kuhusu mpango wowote wa wanamuziki kukutana na rais kwani mpango huo ulifanywa kwa siri kubwa.
“Ninavyofahamu kibinafsi ni kuwa mkutano huo si wa wanamuziki kwa sababu baadhi yetu hatufahamu kuuhusu. Sitahudhuria kwa sababu hakuna mpangilio wowote na sitaki kushirikiana na kikundi ambacho hakina mipangilio,” akasema.
Kwa upande wake, mwanamuziki Joseph Kariuki Wa Kiarutara, alisema mkutano huo unafaa kufutiliwa mbali kwa sababu wasanii wengi hawakufahamu kuuhusu.
Aliongeza kuwa kama utakuwepo, ufanywe katika uwanja wa michezo wa Kasarani ili wote wahudhurie.
Hata hivyo, John De Matthew, ambaye ni miongoni mwa waliokuwa katika mstari wa mbele katika maandalizi ya mkutano huo, alisema mkutano ulikuwa umepangwa mapema na hata rais alifahamu kuuhusu.
“Hakuna vile sote tunaweza kutoshea Ikulu. Lakini kuna mipango ya kuhusisha kila mmoja wetu kabla na baada ya mkutano huo,” akasema.