‘Naibu Rais hajatimiza ahadi za maendeleo kwetu’
Na VIVERE NANDIEMO
VIONGOZI na wananchi wa Migori wamemtaka Naibu Rais William Ruto kutimiza ahadi za maendeleo alitoa kwao alipofanya ziara kadha katika maeneo hayo mwaka wa 2018.
Walisema nyingi za miradi ambayo Dkt Ruto alisema kuwa serikali ya kitaifa itaanzisha katika maeneo kadha katika kaunti hiyo haijaanzishwa, miezi kadhaa baada ya kuzinduliwa.
Mwaka jana Ruto alizuru Migori mara tano, akitoa ahadi mbalimbali za maendeleo. Katika ziara ya hivi punde, miezi miwili iliyopita ambapo alipokewa na Gavana Okoth Obado, alifufua upya ujenzi wa barabara ya Kehencha-Migori-Masara ambayo ilikwama kabla ya kufika katika eneo la Muhuru Bay katika kaunti ndogo ya Nyatike.
Kufikia sasa ujenzi huo haujaanza licha ya Dkt Ruto, wakati huo, kuahidi kuwa mwanakandarasi angeanza kazi Januari mosi mwaka huu.
Wakati wa ziara hiyo Naibu Rais pia aliahidi kuwa serikali kuu itaanzisha ujenzi wa Vyuo vya Kiufundi katika maeneo bunge ya Suna Magharibu na Nyatike. Wakati huo aliwataka wabunge Peter Masara (Suna Mashariki) na Tom Odege (Nyatike) kufika afisini mwake na “kuchukua pesa za kuanzisha miradi hiyo.
“Aliahidi kuanzisha Chuo cha Kiufundi katika eneo la Masara lakini kufikia sasa hajatimiza ahadi hiyo. Tumejaribu kumfikia lakini bado tunasubiri,” Bw Masara akasema.
Katika eneo la Kuria, ambako Dkt Ruto alizuru kwingi, wakazi wamelalamikia kutotimizwa kwa ahadi za maendeleo zilizotolewa kuanzia mwaka wa 2017.
Mnamo Novemba, mwaka 2018 Naibu Rais alifungua rasmi Chuo cha Kiufundi cha Kedenge ambacho alisema kitaanza kuwasajili wanafunzi kuanzia Januari mwaka huu. Alisema kuwa kundi la kwanza la wanafunzi watadhaminiwa na serikali. Lakini miezi miwili baada ya kufunguliwa chuo hicho kingali hakina wanafunzi na hamna shughuli zozote zinazoendelea humo.
Akiwahutubia wananchi wakati huo, Dkt Ruto aliahidi kuwa serikali kuu itatoa ruzuku ya Sh100 milioni kuimarisha miundo msingi katika mji wa Kehancha. Aidha, aliahidi kuwa Wizara ya Afya itapeleka mtambo wa CT scan katika Hospitali ya Rufaa ya Migori. Lakini mpaka sasa ahadi hizo hazijatimizwa.